Watani wa Jadi Kesho Kitawaka Kwa Mkapa, Yanayonogesha Kariakoo Dabi Yapo Hapa-Michezoni leo

Kikosi cha Yanga.

KESHO kutakuwa na mchezo wa watani wa jadi katika Ligi kuu Tanzania Bara ambapo Yanga itaikaribisha Simba.

Simba katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao walikuwa wenyeji wa Yanga, matokeo yalikuwa 0-0.

 

Tukienda kushuhudia mchezo wa mzunguko wa pili unaotarajiwa kufanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar, Yanga wataingia wakiwa na pointi 13 zaidi ya Simba.

 

Kuelekea mchezo huo ambao umekuwa na mambo mengi ndani na nje ya uwanja, Spoti Xtra linakuchambulia yale yanayonogesha dabi hiyo.

 

Morrison kuifunga Yanga

Tangu Bernard Morrison ahamie Simba akitokea Yanga, ameshindwa kuwafunga waajiri wake hao wa zamani akiwa amecheza michezo mitatu dhidi yao.

Katika mchezo uliopita, Morrison wakati anafanyiwa mabadiliko alionekana kugoma kutokana na kuhitaji kucheza zaidi ili awafunge Yanga. Jumamosi hii ana nafasi ya kuonesha kiu yake endapo akipewa muda wa kucheza.

Wachezaji wa timu ya Simba wakifanya yao.

Nabi kukaa jukwaani

Katika mchezo huu, habari mbaya zaidi kwa mashabiki wa Yanga ni juu ya kocha wao mkuu, Nasreddine Nabi kuwa jukwaani wakati timu hizo zitakapocheza.

Nabi anakosekana kutokana na kupewa kadi nyekundu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Geita Gold na kufungiwa mechi tatu.

Tayari amekosekana katika mchezo mmoja dhidi ya Namungo, hivyo imebaki michezo miwili ya kukosekana dhidi ya Simba na Ruvu Shooting.

Swali linakuja, Yanga bila Nabi itaweza kupata matokeo mazuri mbele ya Simba.

 

Haji Manara vs Ahmed Ally

Kuelekea mchezo huo, vijembe, tambo na hamasa zimeonekana kuwa kubwa katika upande wa wasemaji wa timu hizo.

Kwa upande wa Yanga, Haji Manara, ameanza tambo kuelekea mchezo huo kutokana na wao kuwa wenyeji.

Simba wanaye Ahmed Ally, yeye ameanza kutamba kuwa lazima wapate matokeo dhidi ya Yanga.

Mayele na Saido wakifanya yao.

Mayele vs Inonga

Vita kubwa ambayo itakuwa inasubiriwa kuonekana ni kati ya mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele na beki wa kati wa Simba, Henock Inonga Baka maarufu Varane.

Vuta picha katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliozikutanisha timu hizo namna Inonga alivyokula sahani moja na Mayele.

Katika mchezo huo, Mayele alikamatwa haswa na beki huyo ambaye wote wanatokea DR Congo.

Wakati Mayele anafanyiwa mabadiliko, Inonga akamsindikiza na kuonesha ishara kuwa amemdhibiti mshambuliaji huyo kiasi cha kushindwa kutetema.

Mayele ambaye ni kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akiwa nayo 12, atakuwa na kazi moja ya kusaka rekodi ya kuwafunga Simba ndani ya ligi hiyo ikiwa tayari amewafunga Ngao ya Jamii.

 

Mwenyewe ameweka wazi kwamba bado ana deni na Simba, hivyo amejipanga kulilipa. Hapo Inonga atakuwa na kazi kuhakikisha anamzuia tena asifunge.

 

Manula vs Diarra

Ukiwataja makipa bora katika Ligi Kuu Bara, jina la Aishi Manula linaweza kuwa namba moja, msimu huu amepata changamoto kubwa kutoka kwa Djigui Diara wa Yanga.

 

Diarra msimu huu ana clean sheet kumi katika Ligi Kuu Bara wakati Manula akiwa nazo tisa.

 

Vita yao ya rekodi itakuwa kwa kila mmoja kuhakikisha analinda vizuri nyavu zake zisitikiswe na kuisaidia timu yake kupata matokeo mazuri. Manula atakuwa anasaka clean sheet ya kumi kumfikia Diarra, wakati mwenzake akipambana kuongeza gepu.

Msimu huu tayari Simba na Yanga zimekutana mara mbili, Ngao ya Jamii na Ligi Kuu Bara.

Katika mechi mbili walizokutana msimu huu, Yanga ina bao moja, Simba haina.

Mchezo wa kwanza msimu huu, Yanga ilishinda 1-0 dhidi ya Simba. Mechi ya pili Simba 0-0 Yanga.

The post Watani wa Jadi Kesho Kitawaka Kwa Mkapa, Yanayonogesha Kariakoo Dabi Yapo Hapa appeared first on Global Publishers.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post