MTU WA MPIRA: Siyo Simba tu, kila timu Afrika ina figisu



 
NIMEONA kelele za watu mitaani baada ya mechi ya Simba na Orlando Pirates. Kelele kuhusu figisu walizofanyiwa Orlando Bongo.

Kelele nyingi zimekuwepo baada ya kocha msaidizi wa Orlando Pirates kulalamika kuwa hawakufanyiwa uungwana walipokuja kucheza na Simba. Ni kichekesho kweli. Kwa uzoefu wangu katika soka la Afrika, hakuna sehemu rafiki kama Tanzania. Tumejaliwa uungwana na ukarimu uliopitiliza.

Ukarimu ambao timu za nje zinapata Tanzania huwezi kupata popote Afrika. Watanzania tumejaliwa maisha hayo. Tunawapenda wageni kama tunavyojipenda sisi. Timu inayokuja kucheza na Simba hapa Tanzania inaweza kupata mapokezi mazuri kutoka kwa Yanga. Ikaonyeshwa hoteli nzuri ya kulala na namna ya kuifunga Simba. Ndio soka la Tanzania. Mbali na hivyo, Simba inaweza pia kuwapokea wapinzani wao vizuri na kuwakarimu mpaka siku ya mechi. Lakini baadaye timu hiyo ikalalamika.

Tatizo kubwa kwenye soka la Afrika ni timu zinazotaka kupata matokeo makubwa bila kuwa na uwezo. Mfano unakuta timu haina uwezo wa kucheza na Simba lakini inajitutumua. Inatamba kushinda.


 
Kuna timu kama ile Plateau ya Nigeria. Iliondoshwa na Simba kwenye mashindano mwaka juzi. Mechi ya kule Nigeria walifanya figisu nyingi lakini bado walipoteza.

Kabla ya mechi hiyo, Simba walikuwa wanapewa nafasi kubwa. Lakini Plateau waliamini ili kuitoa timu kubwa kama Simba ni kufanya figisu. Ujinga ulioje.

Mwaka jana Simba ililaumiwa kuwa inacheza na majibu ya Covid 19. Baadhi ya timu zikadai majibu yao yanachezewa hapa Bongo. Ni ajabu na kweli.


Lakini zilipokuja timu kubwa kama Al Ahly, Kaizer Chiefs na wengineo hawakuwa na changamoto ya Covid 19. Lakini pamoja na hayo, wote walipoteza mechi zao kwa Mkapa. Unawezaje kukaa pembeni na kusema Simba ilikuwa inafanya figisu za Covid 19? Yaani Simba iwe na figisu hizo halafu ifanye kwa timu ndogo tu?

Nadhani kama ni figisu Simba ingefanya zaidi kwenye hizo mechi kubwa siyo katika mechi ndogo pekee. Yaani Simba iifunge Al Ahly kwa Mkapa bila figisu halafu ihangaike kuifanyia hujuma Orlando Pirates? Ni ajabu kweli.

Kabla hatujalaumu timu kuwa inafanya figisu, kwanza tukubali na kuheshimu uwezo wao. Hapo ndipo tutaelewa ukubwa wa Simba.

Wale Raja Casablanca walilalamika kweli kuwa walihujumiwa pale Cairo na Al Ahly. Wakaapa kulipa kisasi pale Morocco lakini nini kimetokea?


 
Ni kweli Ahly walipewa penalti ya ‘mchongo’ pale Cairo. Ni kweli mwamuzi wa mechi ya kwanza hakuwa mchezoni na alifanya makosa mengi.

Pamoja na kwamba makosa yalikuwa ya mwamuzi, Raja waliilaumu Al Ahly kuwa imefanya figisu. Inachekesha kweli. Nini kilitokea baadaye? Kama walivyopewa penalti pale Cairo, ndivyo hivyo Al Ahly walipewa pale Casablanca. Tofauti tu ni kwamba Ahly walikosa mkwaju huo. Mwisho wa mechi Ahly akapata sare ya goli 1-1 ugenini. Wakasonga mbele. Tatizo ni kwamba Raja walilalamika sana kuhusu hujuma na kushindwa kusema ukweli kuhusu uwezo wa Ahly.

Hilo ndio soka la Afrika. Watu hawataki kusema ukweli kuhusu uwezo, wanalia na figisu.

Wale Orlando hata wacheze mechi kumi na Simba pale kwa Mkapa, hawawezi kushinda hata moja. Simba imetengeneza kwa Mkapa kuwa ngome yao. Wameweka nguvu kubwa. Haikuja bahati mbaya tu. Kuna heshima inabidi tuwape Simba kwa kuweza kutumia vyema uwanja wa nyumbani. Kila timu ya nje ikija Bongo inakuwa na hofu.



 




0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post