Magari ya mizigo, magazeti, IT marufuku kubeba abiria



Magari ya mizigo, magazeti, IT marufuku kubeba abiria
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limepiga marufuku magari yote ya mizigo pamoja na magari yanayokwenda nje maarufu kama IT kubeba abiria.

Aidha limetoa onyo kwa wamiliki ambao wanaingiza magari mabovu barabarani na kusababisha ajali.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa kufunga programu maalumu ya kutoa elimu ya usalama barabarani iliyopewa jina la Mahakama ya Watoto iliyofanyika katika shule za msingi tisa za serikali mkoani Dar es Salaam, Kamanda wa Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa amesema marufuku hiyo inaanza mara moja sambamba na ukaguzi wa magari ambayo hayakuwekwa stika ya nenda kwa usalama barabarani.

Akifafanua kuhusu magari ya mizigo kubeba abiria alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya abiria au wamiliki wa magari hayo kubeba abiria  hivyo katika operesheni iliyoanzishwa na kikosi hicho watakamata magari yatakayobainika kubeba abiria wakati ni maalumu kwa kubeba mizigo.


 
"Tukibaini gari ya mizigo (Lori) limebeba abiria tutalikamata gari pamoja na dereva na wamiliki wa magari hayo, lakini hata magari yanayobeba abiria nayo ni marufuku kubeba mizigo. Tunataka watumiaji vyombo vya moto waheshimu sheria za usalama barabarani ili kwa pamoja tushirikiane kupunguza ajali ambazo zinakatisha maisha ya wananchi na wengine kubakia na ulemavu wa kudumu.

"Kuhusu magari ya IT yanayosafirishwa kwenda nje za nje ya Tanzania nayo ni marufuku kubeba abiria na sheria inawataka kubeba abiria mmoja tu na si vinginevyo na hii  haishii kwenye magari ya mizigo na IT tu bali hata magari yanayobeba magazeti nayo ni marufuku kubeba abiria. Katika hili hatutakuwa na utani, dereva na wamiliki lazima wafuate sheria za usalama barabarani,”alisema.

Alisema iwapo abiria anataka kusafiri anatakiwa kwenda kwenye vituo vya mabasi ya abiria ili kupata usafiri wa uhakika na unaotambulika kwa mujibu wa sheria.


Kuhusu makontena au mizigo ambayo hayafungwi vizuri na kusababisha ajali, alisema madereva na wahusika wanatakiwa kuhakikisha wanafunga mizigo ili kuwa salama wakati wote wa safari na kuongeza  kuwa leo yeye(Mutafungwa) na maofisa wake watakutana na madereva waliopo Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumza na kukumbushana wajibu wa kufuata sheria za usalama barabarani.

Akizungumza programu ya usalama barabarani iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Shirika la Amend, Kamanda Mutafungwa alisema programu hiyo ni mwendelezo wa kufikisha elimu ya usalama barabarani na kupitia programu hiyo kuna madereva ambao watakuwa mabalozi katika kuhamasisha kuzingatiwa kwa sheria za barabarani.

Naye  Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo mbali ya kutoa shukrani kwa Shirika la Amend kwa kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi, alisema suala la ulasama barabarani ni jukumu la kila mwananchi na wote wanatakiwa kufuata sheria bila shuruti.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za jeshi hilo zinaonesha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2021 watu 1,245 walipoteza maisha yao na wengine 2,023 walijeruhiwa kutokana na ajali za barabarani."Kati ya takwimu hizo wanafunzi 56 walipoteza maisha na wengine 65 walijeruhiwa”.


 
Awali Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania, Simon Kalolo akizungumzia programu ya Mahakama ya Watoto alisema lengo ni kuendelea kufikisha elimu ya usalama barabarani kwa jamii ya Watanzania



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post