Wafunguka RPC aliyetamani cheo cha Sirro




WADAU wametoa maoni yao juu ya kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera (RPC) Wankyo Nyigesa, kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kumteuwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania haliyakuwa (IGP) Simon Sirro bado anaihudumia nafasi hiyo.

Baadhi walisema siyo jambo baya kwa mtu kutamani cheo fulani  huku wengine wakisema siyo sawa kutamani nafasi ya juu wakati aliyonayo hajaifanyia kazi ipasavyo.

Mratibu wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumo, alisema mtu kutamani cheo cha juu siyo dhambi bali inaweza kutafsiriwa tofauti endapo atatumia njia za hujuma kupata nafasi anayoitamani.

“Siyo vibaya kuomba kuteuliwa, huwenda kuna kitu kakiona kuwa hakiko sawa na kufikiri kuwa endapo atapatiwa nafasi hiyo anaweza kukirekebisha hivyo huo ni ujumbe kwa IGP aliyopo,” alisema Olengurumwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema misingi ya kiutendaji kazi au cheo cha kuteuliwa hakiombi ila Rais humteua mtu pale atakapoona kuwa anafaa.


 
“Watu wote hawawezi kuwa nafasi za juu usitamani cheo kikubwa wakati katika nafasi uliyopo bado hujatatua yaliyopo, katika mkoa alipopelekwa kuna mambo mengi ya kipolisi hayapo sawa hivyo tulitegemea angewaambia wanaKagera kuwa huko anakokwenda atafanya nini kutatua changamoto zilizopo,” alisema Anna.

Akizungumza jana Kibaha Mkoani Pwani wakati wa sherehe za kumuaga baada ya kuhamishwa katika mkoa huo na kupelekwa Kagera RPC Nyigesa, alisema moja ya malengo yake na ndoto zake kubwa ni kuteuliwa kuwa Mkuu wa Polisi nchini (IGP) na anatamani Rais amteue huku akiahidi kuwa atafanya kazi kubwa.

Alibainisha kuwa awali alikuwa anajiandaa kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Kamishna wa Zanzibar, lakini baada ya nafasi hizo kuchukuliwa sasa anajiandaa kuwa IGP, na aninaamini kwamba Rais Samia anayasikia maombi yake.

“Siku moja tafadhali niteue kuwa IGP, mimi naamini nitafanya makubwa, huwa ninaomba sana Mama (Rais) siku moja aniote tu halafu anitamke tu niwe IGP, Mimi nitamuomba nifanye miaka mitatu halafu nimwambie Mama mimi nakukabidhi naondoka unaonaje hapo,” alisema Nyigesa.

“Binadamu lazima uangalie mbele, natamani kuwa IGP, najua IGP aliyopo Sirro hajafanya makosa anafanya mazuri, lakini mimi nitafanya mazuri zaidi, matarajio yangu ni hayo, unajua binadamu lazima uwe na malengo ya mbele, uwe na ndoto kubwa, huwezi tu kuwa una malengo ya kwamba nitaendeela tu kuwa RPC …mimi nataka kuwa nafasi za luu, ili nifanye makubwa kwa faida ya Watanzania wengi kuliko wa mkoa mmoja,” alisema Nyigesa.

Aliongeza kuwa anaamini siku moja Rais atakapomuona vizuri anaweza kumpa U-IGP na matamanio yake ni kuhudumu katika nafasi hiyo, na alimuhakikishia mkuu huyo wa nchi kuwa endapo atamuona anafaa na kumteua atakuwa amepata mtu sahihi kwa wakati sahihi.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post