Siri ya Mti wa ‘Mdigrii’ Kwa Wanafunzi Chuo Kikuu UDSM Mlimani






Ni eneo maarufu na pengine miaka yako ya kuwa chuoni inaweza ikawa na walakini kama hukuwahi kukanyaga eneo hilo.

Unaweza usifike hapo, lakini kwa hali ilivyo, lazima ulijue kwa kuwa ni miongoni mwa maeneo machache yanayotajwa kuwa alama muhimu ya chuo hicho.

Katika eneo hilo ndipo uliposimama mti mkubwa, ukiwa na matawi makubwa kila upande ukitoa kivuli mwanana kwa wakaao chini yake. Ni mithili ya mabawa ya kuku anapowakumbatia vifaranga.

Ni mti uitwao ‘ mdigrii’ uliopo kampasi kuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Simulizi ya kuvutia

Hadithi kuhusu mti huu zinavutia. Haijulikani nani aliupanda, lini na kwa sababu gani, lakini leo umebeba siri kwa jamii ya chuo hicho.

Moja ya simulizi mashuhuri kuhusu mti huo ni ile inayodaiwa na baadhi ya wanafunzi kuwa ukisoma katika mti huo, una uhakika wa kuja kuitia kibindoni shahada yako.

Mmoja wa wahadhiri chuoni hapo, Dk Dotto Paul, anasema miaka ya 1990 mti huo ulipokuwa mkubwa na ukiwa jirani na ukumbi maarufu wa Nkrumah, wanafunzi walipenda kukaa chini yake wakitafuta kivuli na upepo.


Awali hapakuwa na viti wala meza za simenti maarufu kama ‘vimbweta’. Iliwalazimu wanafunzi kuhamisha viti kutoka madarasa ya karibu ili kwenda kukaa hapo kujisomea na kujadiliana.

“Ilianza kama mzaha inasemekana baadhi ya wanafunzi wakikaa hapo walianza kutaniana kwamba usipokaa chini ya mti huo huwezi kutunukiwa digirii.

‘‘Ilienda hivyo hadi vilipowekwa vimbweta bado wanafunzi waliendelea kutaniana na kufanya jina hilo kuota mizizi na kufanya hata baadhi yao kuamini kuwa jina halisi la mti huo kuwa ni mdigirii,”anasema.

Dk Paul anayesimamia kitengo cha mawasiliano chuoni hapo anasema kingine kilichofanya jina la mdigrii kushika kani, ni tabia yake ya kudondosha majani wakati wa msimu wa kiangazi chuo kinapofungwa na kisha kuchanua majani chuo kinapofunguliwa na ndani ya miezi ya mahafali ambayo wanafunzi hutunukiwa shahada zao.


“Mti huu una jina lake kitaalamu, hilo la mdigrii limekuwa tu ni jina pendwa, Hapakuwa na kikao rasmi juu ya kuuita mti huo mdigirii,”anaongeza kusema.

Alama muhimu ya chuo

Kwa upande wake, Dk Faraja Kristomus anasema mti huo unaosadikika kuwa unaweza kuishi hata kwa miaka 300, ni alama ya kudumu ya chuo hicho ambacho kwa sasa kinazidi kupanuka.

‘’ Sifa kubwa ya mti wa mdigrii ni kuwa ulikuwa unadondosha majani kipindi cha kiangazi chuo kinapofungwa na majani kuchipua kipindi ambacho miaka ya nyuma kilikuwa cha kutunuku shahada au digrii. Ndio asili ya kuitwa mdigrii,’ anafafanua.

Kusisitiza umuhimu wa mti huo, uongozi wa chuo kupitia tovuti yake, www.udsm.ac.tz, unautaja mti huo kama mojawapo ya alama tisa zinazokitambulisha chuo hicho, ukiwamo ukumbi maarufu wa Nkrumah unaoelezwa kuwa ni kielelezo cha taaluma, ukombozi na maendeleo.


Kwa mujibu wa Dk Paul, alama nyingine chuoni hapo ni daraja maarufu la taaluma (academic bridge), linalosimama kama kielelezo cha uhusiano wa taaluma na maisha ya wanafunzi chuoni hapo.

Kutoka wanafunzi kuhamisha viti na kwenda kujisomea chini ya mti huo, hivi sasa mandhari ya mdigrii yanavutia.

Sio tu kumejengwa vimbweta (viti na meza za zege), kwa ajili ya kuwasitiri wanafunzi, lakini usiku mahala hapo panaendelea kung’aa kwa taa zilizowekwa kuzunguka eneo hilo.

Wanafunzi wanauzungumziaje?

Mwajuma Zuberi, anayesoma mwaka wa tatu shahada ya awali ya sayansi ya siasa na utawala wa umma, anasema kuwa huwezi kuwa mwanafunzi wa chuo hicho na ukahitimu bila hata siku moja kukaa katika mti huo kujisomea.

“Hili eneo na mti huu wa mdigirii ni kama urithi wa wanafunzi chuoni hapa, kwani ni eneo tulivu kujisomea, lina vimbweta vya kutosha na lipo jirani na madarasa ambayo wanafunzi wanatumia kusomea,”anaeleza.


Naye Moses Matula anayesomea shahada ya awali ya sayansi katika kemia, anasema kutokana na mazingira chini ya mti huo kuwaruhusu wanafunzi kusoma vyema na hata kufanya vizuri, kumefanya baadhi ya wanafunzi kuwa na imani kuwa ukisoma chini ya mti huo utafaulu.

“Mazingira ya Dar es Salaam yana joto sana, hivyo sehemu kama hii yenye upepo wa kutosha kivuli na utulivu wa hali ya juu humfanya mwanafunzi kusoma vizuri huku akili yake ikiwa imetulia, ndio maana ukija katikati mwa ‘semester’ kipindi cha mitihani utakuta wanafunzi wengi sana wakiwa hapa wanajisomea”anasema.

Mti wa mijadala

Wakati wengine wakipendelea kujisomea chini ya mti huo, Magreth Mbayi, anayesomea shahada ya awali katika elimu anasema eneo hilo linapendwa kwa ajili ya majadiliano ya masomo miongoni mwa wanafunzi.

“Hapa wanakuja kujisomea na kufanya majadiliano wanafunzi wa miaka yote ya masomo kutoka kozi mbalimbali, hivyo hata ukiwa kuna sehemu labda hujaelewa ni rahisi kumuuliza yule aliyekutangulia, akakusaidia na hata kukupatia maarifa mapya yatakayokusaidia kwa namna moja au nyingine kufanya vizuri,”anasema.

Laiti ungezungumza

Nje ya kujisomea na masuala mengie ya kitaaluma, mdigrii umebeba siri nyingi za wanafunzi kama anavyosema mhitimu Musa Ali:

‘ Ni mti unaotumika kwa malengo tofauti miongoni mwa wanachuo. Wengine waliutumia kujiandaa na mitihani, wengine kuteta na wapenzi wao. Wapo pia wanaoutumia kuvinjari na wengine kutafakari maisha ya kampasi.’’

Si Udsm pekee

Ukongwe wa Udsm, unakifanya kuwa kiigizo cha vyuo vingi nchini. Kwa mfano, kuna misemo ambayo asili yake ni chuoni hapo, lakini sasa imekuwa misemo ya kitaifa ikitumika vyuo mbalimbali.

Achana na msemo kama ‘ desa’ hata mdigrii uliopo hapo, sasa umepata pacha wake. Kuna mdigrii mwingine katika Chuo Kikuu cha St John kilichopo jijini Dodoma.

Mhadhiri wa masuala ya jiografia na maliasili chuoni hapo, Dk Fadhili Bwagalilo anasema taarifa zilizopo ni kuwa mti huo ulikuwa hapo tangu enzi za ukoloni.

“Inasemekana enzi hizo kabla na enzi za ukoloni eneo la mti huu lilikuwa likitumika kama eneo la kuhukumia watu wanaotenda makosa mbalimbali, hivyo ninaweza kusema ulikuwepo kabla ya chuo kujengwa,”anasema.

Anasema mdigrii uliopo katika chuo hicho ni mti aina ya mkuyu ambao mara nyingi huota katika sehemu zenye maji mengi na ulipewa jina hilo kwa kukopa kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

“Pale katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuna mti mkubwa sana ambao ulibatizwa jina hilo la mdigrii kutokana na wanafunzi kupenda kukaa chini ya mti huo kujisomea pamoja na kufanya kazi mbalimbali za darasani pamoja na majadiliano ya kimasomo,”anasema na kuongeza:

“Kutokana na mti huu uliopo chuoni hapa kuwa mkubwa na wenye kivuli cha kutosha hivyo kutengeneza mazingira mazuri ya wanafunzi kujisomea ndio chanzo cha kupewa jina la mdigrii bila kujali ni aina gani ya mti.’’

Mti wa imani

Baadhi ya mitandao inautaja mti wa ‘ ficus religiosa’ kuwa na uhusiano na baadhi ya imani zikiwamo za dini kama Ubudha, Uhindu na Ujai (Jainism) iliyotamalaki zaidi katika nchi za bara la Asia.

Ndio maana mti huo unatajwa kuwa maarufu katika maeneo kama kusini magharibi mwa China, India, Nepal, Burma, Sri Lanka na baadhi ya maeneo ya Indochina.

Unatajwa kuwa na uwezo wa kufikia urefu wa mita 30 kwenda juu, ukiwa na majani mapana na matawi imara yanayoweza kusambaa zaidi.

Ni mti wenye nasaba kifamilia na miti kama vile mtini na mforosadi.

Katika maelezo mengine yakiwamo yaliyomo kwenye mtandao wa wikipedia, miti ya famili hiyo inaweza kuishi kwa miaka 900 hadi 1,500, huku ukiaminika kuwa na utukufu wa kiimani.

Katika majimbo ya Odisha na Haryana nchini India, mti huo umepewa hadhi ya kuwa mti maalumu wa taifa.






0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post