Shahidi mwingine akana kumfahamu Sabaya




Shahidi mwingine akana kumfahamu Sabaya
MSHITAKIWA wa nne katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake sita, John Aweyo (49) amedai hamfahamu Sabaya na washitakiwa wengine.

Shahidi huyo alidai jana katika Mahakama ya Mkoa wa Arusha kuwa kwa mara ya kwanza alikutana na washitakiwa wenzake mahakamani na wengine katika Gereza la Kisongo mkoani Arusha.

Aweyo alisema yeye ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba za aina zote. Alidai Januari 22, mwaka jana alikuwa nyumbani, baadaye katika kibanda chake cha nguo hadi saa 3 usiku na akarudi nyumbani.

Awali, shahidi wa tatu katika kesi hiyo, Enock Mnkeni (41) alidai Januari 22, mwaka jana alikuwa Arusha, lakini alikuwa hamfahamu Sabaya.


 
Mnkeni alidai mahakamani kuwa kwa mara ya kwanza alimfahamu Sabaya Juni 4, mwaka jana alipofikishwa naye kizimbani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Shahidi huyo ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo alidai hayo wakati akihojiwa na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Arusha, Richard Jacopiyo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda.

Mnkeni alidai hakukamatwa na maofisa wa Takukuru Dar es Salaam kama shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri alivyodai, bali alipigiwa simu na maofisa wa taasisi hiyo wa Arusha kutakiwa kuripoti ofisini kwao na alifanya hivyo.


Shahidi huyo alikiri kuwa namba ya simu 0759 978686 imesajiliwa kwa jina lake na alikiri kuwasiliana na namba ya simu 0758 707171 iliyosajiliwa kwa jina la Lengai Ole Sabaya siku ya Januari 22, mwaka jana, lakini aliyekuwa akizungumza kwenye simu ilikuwa sauti ya kike na alikuwa wakitafutana kwa ajili ya kufanya biashara ya mazao.

Shahidi huyo alikiri mahakamani hapo kuwa shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri aliieleza mahakama kuwa yeye Mnkeni, Sabaya, Oweyo (49) na Silverster Nyengu (26) walikamatwa Dar es Salaam na maofisa wa Takukuru.

Alidai alikana kukamatwa Dar es Salaam, bali aliitwa Takukuru Arusha na kukaa rumande kwa siku saba kabla ya siku ya nane ya kufikishwa mahakamani na washitakiwa wengine ambao aliwajua siku hiyo.

Akihojiwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Tasila Asenga kuwa kama ana utaalamu wa kielektroniki wa kutambua ama kujua kamera za CCTV zinapofanya kazi, shahidi huyo alidai kutojua hilo.


 
Asenga alimkabidhi kielelezo P3 taarifa ya mawasiliano kutoka Kampuni ya Vodacom ikionesha mawasiliano ya simu yake 0759 978686 iliyosajiliwa kwa jina lake ikiwa inawasiliana mara kwa mara na namba ya simu 0758 707171 iliyosajiliwa kwa jina la Lengai Ole Sabaya, siku ya Januari 22, mwaka jana na kukiri kuwasiliana na namba hiyo.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post