Putin Ahofia Kupewa Sumu....Afukuza Wafanyakazi Zaidi ya 1000


Wakati mapigano yakiwa yanaendelea nchini Ukraine, zimeibuka taarifa za kiintelijensia zikidai Rais wa Urusi, Vladimir Putin yupo hatarini kuuawa kwa kupewa sumu.

Duru za kiintelijensia zinasema kuwa Rais Putin amekuwa anaishi kwa kuwahofia zaidi watu wake wa karibu na hivi karibuni, amefanya mabadiliko kwa kuwaondoa wafanyakazi wake wa karibu 1000 kutoka katika idara mbalimbali na kuweka wengine wapya.

Maafisa wakubwa nchini Urusi wanasadikika kupanga njama za kumuua Rais Putin na kumsimika mrithi wake ambaye atafufua uhusiano wa kibiashara na nchi za Magharibi.

Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha intelijensia wa Ukraine, kundi la viongozi wa ngazi za juu wa Urusi wenye ushawishi mkubwa wanafikiria kuhusu njia mbalimbali za kutumia kumuua Rais Putin kwa njia yoyote ile hasa sumu.

Imeelezwa kuwa mauaji kwa kutumia sumu ndiyo njia maarufu zaidi nchini Urusi na mtekelezaji wa mauaji hayo ni yeye mwenyewe Rais Putin ambaye inadaiwa alihusika katika njama za mauaji ya Alexander Litvinenko mwaka 2006 ambaye alikuwa ni Afisa wa Idara ya Usalama wa Urusi.

Idara ya Usalama wa Taifa nchini Ukraine imesema kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Urusi, Oleksandr Bortnikov ndiye anayeripotiwa kuja kuwa mrithi wa Putin endapo juhudi zao za kumuua rais huyo zitafanikiwa.

Mkuu huyo wa Idara ya Intelijensia wa Ukraine alinukuliwa akisema:
“Inaeleweka kuwa Bortnikov pamoja na maafisa wengine wakubwa kwenye Serikali ya Urusi wanafikiria njia mbalimbali za kumuondoa Putin madarakani, hasa sumu, ugonjwa wa ghafla au njia nyingine yoyote ile.”


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post