WAKATI Ligi Kuu Bara zikibaki takribani mechi 18 kwa kila timu kucheza kumaliza msimu huu, vinara wa ligi hiyo, Yanga SC, wanaonekana kuwa na wakati mzuri wa kuwa mabingwa.
Kasi yao katika ligi msimu huu, inawafanya wengi waamini hivyo kwani ndiyo timu pekee hadi sasa haijapoteza mechi ikishuka dimbani mara 18, huku ikikusanya alama 48. Imewazidi mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba kwa alama 11 ambayo yenyewe imecheza mechi 17 na kukusanya alama 37.
Aprili 30, mwaka huu, timu hizo zitapambana Uwanja wa Mkapa, Dar katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara. Kiungo wa zamani wa Simba raia wa Ghana, James Kotei, amezungumzia ubora wa Yanga ilionao msimu huu, huku akisema wanaweza kuwavua ubingwa Simba.
“Kwanza nafurahi kuona ligi ya msimu huu ikiwa na ushindani mkubwa, binafsi nafurahi kuona Yanga ikitoa changamoto kubwa kwa Simba katika vita ya kuwania ubingwa, inaweza kufanikiwa. “Ushindani huu una faida kubwa sana kwenye kukuza thamani ya ligi, inawafanya wachezaji pia kupambana na kukuza viwango vyao ambavyo baadaye inakuwa faida kubwa kwa taifa timu ya Taifa.
“Jambo lililowazi ni kuwa, Yanga ya msimu huu inaonekana kuwa bora zaidi kulinganisha na msimu uliopita. “Katika hili nadhani uongozi wao unapaswa kupongezwa kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kuwa na timu waliyonayo, ukitazama walipotoka na kuwa na timu hii si rahisi,” alisema Kotei.
STORI NA JOEL THOMAS
Post a Comment