Msemaji wa Klabu ya Young Africans Haji Sunday Manara amewataka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kupuuza mambo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii na katika baadhi ya vyombo vya habari, yenye lengo la kuwatoa kwenye malengo yao Msimu huu 2021/22.
Young Africans imeweka dhamira ya kutwaa Taji la Ligi Kuu Tanzania Bara Msimu huu, baada ya kulikosa kwa misimu minne mfululizo kwa kushuhudia likienda kwa Watani zao wa Jadi Simba SC.
Manara amesema anaamini kuna makusudi inafanywa na baadhi ya watu ili kuikwamisha Young Africans isifikie lengo lake, hivyo amewasihi Mashabiki na Wanachama kuendelea kuwa kitu kimoja ili kufanikisha wanalolikusudia.
“Wananchi wenzangu, interest yetu iwe kushinda Championship msimu huu, iwe kushinda FA na iwe kukamilisha Transformation yetu, mengine ni ya kupuuza.”
“Nipo hapa kushirikiana na nyinyi kushinda Mataji, sipo hapa kujibizana na mtu, tuendelee kuwasamehe wanaotaka vurugu na malumbano coz bila kumtaja Haji kwa ubaya atamtaja nani?”
“Umoja wetu ndio nguvu tuliyonayo kwa sasa, tusijitoe relini kisa choyo, chuki na roho mbaya, tuwekeni maslahi mapana ya hii Taasisi.”
“Once again nawashukuru Wanayanga, mmenirudishia umri wangu nyuma, hamjawahi kuniacha toka nilipokuja Club hii kubwa, mwenzenu nimejaaliwa Moyo mgumu wa kustahmili kashfa na karaha na hiyo inanipa ujasiri mkubwa katika kazi zangu.” Amesema Haji Manara
Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 48, huku ikiiacha Simba SC yenye alama 38 kwa tofauti ya alama 11, na tayari imeshatinga hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Young Africans itacheza dhidi ya Geita Gold FC katika mchezo wa Robo Fainali ‘ASFC’ mapema mwezi April, Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.
Post a Comment