MUHOOZI Kainerugaba, aliyezaliwa Aprili 1974, jijini Dar es Salaam akiwa ni mtoto kifungua mimba wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni. Leo hii aking’ara vilivyo begani kijeshi.
Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la ‘The UG Standard la Uganda’, akiwa mdogo Kainerugaba, alisoma Tanzania, baadaye alijiunga na shule ya Mount Kenya Academy iliyoko Nyeri Kenya na baadaye akaendelea na masomo nchini Sweden.
Ilipofika mwaka 1999, aliandikishwa katika Jeshi la Uganda la UPDF, akiwa ofisa mwanafunzi au ‘ofisa cadet’ na kuhitimu 2000.
Kijeshi amezama darasani nchini Uganda, pia kwenye masuala ya kijeshi, amepitia Chuo cha Kijeshi cha Misri (Egyptian Military Academy) na kujifunza zaidi.
Pia, baadaye akajiongeza kitaalamu, 2007 akijiunga Marekani katika chuo kiitwacho US Army Command and General Staff College at Fort Leavenworth, Kansas, alikohitimu, mnamo Juni 2008.
Safari ya maisha ya Kainerugaba, inatajwa wakati akisoma sekondari aliwahi ‘kuokoka’ enzi za ujana.
Kwa sasa anatumikia Kikosi Maalumu cha Ulinzi wa Rais, pia kikitajwa kutumika kwenye operesheni mbalimbali, zikiwamo za kuhakikisha amani na usalama kwenye serikali ya nchi hiyo.
Ramani ya maisha ya Kainerugaba kijeshi, inatajwa ilianza kubadilika kati ya mwaka 2008 hadi 2017, alipopandishwa cheo na kuteuliwa kuwa mshauri wa Museveni kiusalama.
Hata hivyo, wako watabiri wenye dhana kisiasa walioona katika sura ya kuandaliwa kuchukua uongozi wa nchi.
Lakini si Kainerugaba pekee ambaye yuko kwenye uongozi hata mama yake, Janet Museveni, ni Waziri wa Elimu na Michezo tangu mwaka 2016.
Luteni Jenerali Kainerugaba Muhoozi, amekuwa gumzo nchini mwake tangu ilipodaiwa kuwa anapikwa ili amrithi baba yake Yoweri Museveni uraisi wa Uganda, ni katika harakati hizo Mwaka 2017 Rais Yoweri Museveni, alimpandisha cheo mwanawe na kufikia cheo cha pili kwa ukubwa zaidi jeshini, kutoka cha awali Meja Jenerali
na kufikia Luteni Jenerali katika Jeshi la Uganda.
Kainerugaba, ambaye sasa ana umri wa miaka 48 yupo cheo kimoja nyuma ya baba yake, ambaye ni Jenerali. Huku ndani ya muongo mmoja akipitia ngazi kadhaa za vyeo nchini Uganda. Kwa sasa ni Mkuu wa Kikosi Maalumu cha Ulinzi wa Rais.
Awali, alishahudumu kuwa Mshauri wa Rais wa Operesheni Maalumu.
Kupanda kwake vyeo kwa kasi kuliripotiwa na shirika la habari BBC, ikioanishwa na lugha ya wakosoaji kutoka jicho la kisiasa.
Uganda ilifanya uchaguzi wake mnamo Januari mwaka jana na Rais Museveni akasimama peke yake kugombea urais na kuendelea kukaa Ikulu tangu alipoingia madarakani mwaka 1986.
Museveni mwenye umri wa miaka 78 sasa, amekuwa akilaumiwa kwa kuwapo madarakani kwa miongo mitatu na nusu.
MTOTO AKANUSHA
Hata hivyo, Jenerali Kainerugaba amekuwa akikanusha kuwa ana mipango ya kujiingiza kwenye masuala ya siasa.
Mwaka 2013 kipindi hicho akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali na Mkuu wa Vikosi Maalumu, Luteni Jenerali Muhoozi, akalitolea ufafanuzi kwa taarifa rasmi: "Uganda siyo ufalme ambao uongozi unarithiwa kutoka baba hadi kwa mwanawe. Uamuzi wa kuamua ambavyo Uganda itaongozwa ni jukumu la wananchi wenyewe wala sio mtu mmoja kama wanavyosema baadhi ya watu.''
Ni baada ya magazeti ya Daily Monitor na Red Paper mwaka 2013, kuandika taarifa zenye madai inasukwa mipango kumrithisha mamlaka ya uongozi kutoka kwa baba yake, Rais Museveni.
Waraka huo uliandikwa na Jenerali, David Sejusa, aliyedai kuwa Museveni anamuandaa mwanawe kumrithi, ingawa madai hayo yalikosolewa na majenerali wengine jeshini.
Kamanda huyo wa kijeshi alikimbilia uhamishoni nchini Uingereza. Muda mfupi baadaye, BBC iliripoti magazeti hayo mawili, pia vituo viwili vya redio vilifungiwa kwa siku 10 kwa kuchapisha barua hiyo.
Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, hadi sasa awajibika katika eneo la Mshauri wa Rais Museveni wa masuala ya ulinzi, akiwa ndani ya kitengo kinacho husika na kumlinda Rais wa Uganda hadi sasa.
Hivi karibuni Rwanda na Uganda zimesuluhisha uhusiano kati yao uliokuwa unasuasua tangu mwaka 2017, kutokana na madai ya Uganda kuwakamata raia kadhaa wa Rwanda wanaoishi nchini humo, ikidaiwa kuwa ni hujuma mbaya.
Ni mzozo uliosababisha kufungwa kwa mpaka uitwao Gatuna/Katuna unaounganisha nchi hizo mbili, hata hivyo mambo yakasawazishwa baada ya Rais Paul Kagame wa Rwanda kukutana na mjumbe wa Rais Museveni, Jenerali Kainerugaba na sasa mambo ni shwari.
Ilikuwa mjadala ambao ulitia fora katika siasa baina ya pande hizo, mara zote, mjumbe huyo wa Rais Museveni kumuita Rais Kagame, kwa jina la kiheshima ‘baba mdogo’ akitoa heshima ya uhusiano uliokuwepo kati yao.
Kwa mujibu wa BBC na The Monitor ya Uganda.
Post a Comment