PENDO Athumani (3), mkazi wa kata ya Nyihogo Manispaa ya Kahama, amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kufungwa katika mfuko wa sandarusi na kutupwa nyuma ya nyumba aliyokuwa akiishi na mama yake mzazi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyihogo, Idd Mitimingi, alibainisha hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusiana na mauaji hayo ambayo yalitokea Februari 9, mwaka huu.
Alisema mtoto huyo aliokotwa akiwa amekufa siku moja baada ya kupotea na kwamba mzazi wake alikuwa akiendelea kumtafuta.
Mitimingi alisema, awali alipatiwa taarifa za kupotea kwa mtoto huyo kabla ya kupatikana akiwa amefariki dunia na baada ya kukagua mwili huo ulionyesha dalili za kunyongwa.
“Mtoto bado mdogo na alikuwa bado anahitaji malezi ya baba na mama. Alipotea katika mazingira ya kutatanisha kwa mujibu wa mama yake mzazi lakini amepatikana akiwa amekufa tena kwa kufungwa kwenye sandurusi na kutupwa nyuma ya nyumba aliyokuwa akiishi,” alisema Mitimingi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Joseph Paulo, alithibitisha kutokea mauaji hayo na kwamba mtoto huyo alinyongwa na watu wasiojulikana na kutupwa.
Alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili kuwabaini wahusika waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Post a Comment