Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Benjamin Kuzaga akizungumza na waandishi wa habari.
Hanang’. Mkulima wa kijiji cha Measkroni Wilayani Hanang' Mkoani Manyara, Isack Marko (21) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua Shamba Awe (56) mkazi wa kata ya Gisambalang kwa kumpiga na mpini wa jembe kichwani.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, (ACP) Benjamin Kuzaga akizungumza mjini Babati leo Februari 13 amesema tukio hilo limetokea Februari 11 kwenye Kijii cha Waranga Kata ya Gisambalang.
Kamanda Kuzaga amesema Marko anatuhumiwa kumuua Awe kwa kumpiga kichwani na kitu butu na kusababisha kifo chake papo hapo.
Amesema chanzo cha kifo hicho ni ugomvi ulioanzia shambani wakati wakulima hao walipokuwa wanashirikiana kulima.
"Walitofautiana lugha ndipo wakaanzisha ugomvi na ghafla Marko akampiga kichani na mpini wa jembe, Awe aliyefariki dunia papo hapo," amesema kamanda Kuzaga.
Amesema mtuhumiwa huyo alijaribu kutoroka kwa kutaka kukimbia baada ya tukio hilo ila alikamatwa na polisi wakishirikiana na wananchi wa eneo hilo.
“Tunaendelea kutoa wito kwa jamii kutojichukulia sheria mkononi na badala yake waendelee kushirikiana na polisi kutoa taarifa za kihalifu na uhalifu,” amesema kamanda Kuzaga.
Amesema taarifa hizo zikitolewa zitashughulikiwa na kuhakikisha kuwa mkoa wa Manyara unakuwa ni mahali salama kwa yeyote anayefika.
Post a Comment