Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limesema chanzo cha ajali iliyotokea leo wilayani Busega mkoani Simiyu na kusababisha vifo vya watu 14 ni mwendokasi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Blasius Chatanda amesema kabla ya ajali hiyo kutokea gari iliyokuwa imebeba waandishi wa habari iligonga lori aina ya Tata na kupoteza uelekeo kisha kuparamia dalalada iliyokuwa nyuma ikitokea mkoani Simiyu kwenda jijini Mwanza.
"Baada ya kuigonga ile Tata ilimpotezea uelekeo ambao sasa katika kuhangaika nayo ilitaka kumpeleka kwenye korongo kwa sababu kulikuwa na korongo akairudisha barabarani ikamshinda ndipo akaigonga gari nyingine aina ya Toyota Hiace ambayo ndani yake kulikuwa na abiria waliokuwa wakitoka Simiyu kwenda Mwanza," amesema Kamanda Chatanda
Wakati huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel akizungumza muda mfupi baada ya kupokea miili ya marehemu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure, amesema ajali hiyo imesababisha vifo vya watu 14 miongoni mwao ni waandishi wa habari 5 wa jijiji Mwanza.
Gabriel amesema baada ya kupokea miili hiyo, mkoa unapanga kuaga miili ya marehemu hao kesho Jumatano Januari 12, 2022 katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kabla ya familia kuichukua kwa ajili ya kuendelea na taratibu za maziko.
"Nimemuomba mkuu wa Wilaya ya Nyamagana katika kamati ya maandalizi iangalie uwezekano wa kutumia uwanja wa Nyamagana kwa ajili ya kuwapatia heshima yao ya mwisho wapendwa wetu," amesema Gabriel
Post a Comment