Simba, Red Arrows Simba, Red Arrows kufa au kupona




Simba, Red Arrows Simba, Red Arrows kufa au kupona
SIMBA leo itakuwa ugenini kutafuta ushindi katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Mashujaa.

Mchezo huo una umuhimu kwao kushinda au kupata sare matokeo yatakayowapeleka moja kwa moja hatua za makundi, lakini ikiwa watapoteza kwa mabao kuanzia manne utakuwa ndio mwisho wao.

Wekundu hao wanashuka dimbani wakiwa na faida ya ushindi wa mabao 3-0 walioshinda katika mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin, Mkapa. Iwapo Simba itafuzu hatua ya makundi itakuwa imeweka historia mpya katika michuano hiyo kwani rekodi zake zinaonesha imekuwa ikiishia hatua za awali.

Simba miaka ya karibuni tayari iliweka rekodi Ligi ya Mabingwa baada ya kufanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali mara mbili kwa hivyo, kama na Shirikisho itaingia hatua ya makundi na kuvuka itakuwa ni heshima nyingine kwao wenyewe na taifa.


 
Kwa upande wa wapinzani wao, hawana rekodi ya juu katika michuano hiyo zaidi ya kuishia hatua za awali huku wakiwa wameshiriki mara chache tofauti na Simba wanaoonekana wababe. Lakini ili kufikia huko ni muhimu wekundu hao kupambana kufa au kupona kwa kuhakikisha inapata matokeo mazuri.

Ushindi kwao na kufuzu itakuwa ni heshima na rekodi mpya kwa Kocha wao Pablo Franco anayefanya kazi kwa mara ya kwanza katika timu ya Afrika kwa hiyo atajenga wasifu bora. Akizungumzia mchezo huo jana Pablo alisema wanahitaji kuwa makini muda wote kwa kuhakikisha wanatumia nafasi wanazopata kwa ufanisi.

Kocha Pablo alisema mchezo huo unaweza kuwa mgumu kwani wapinzani watakuja kwa nguvu ya kutaka kupindua matokeo, ila wao wana wachezaji wazuri na watacheza kwenye uwanja mzuri hivyo, ni lazima wafikirie ushindi.

“Wapinzani wataingia kwa nguvu kuhakikisha wanashambulia kupata mabao, wao hawana cha kupoteza na watakuwa na faida ya kucheza nyumbani hivyo, tunapaswa kuchukua tahadhari lakini sitaki kwenda hatua inayofuata kwa kuteseka au kupoteza”alisema.

Pablo alitoka kuiongoza Simba kushinda mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Geita wa mabao 2-1 ushindi uliompa taswira halisi ya kikosi chake namna ya kujipanga kwa mchezo huo. Simba sio wageni wa michuano ya kimataifa wanajua namna ya kuziepuka fitna za ugenini hivyo, huenda kama walivyofanya msimu uliopita ikiwa wamejipanga vizuri basi wanaweza kupata matokeo.

Lakini hawapaswi kuwadharau wapinzani wao kwasababu watakuwa nyumbani na watatafuta kila namna ili kupindua meza.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post