Ripoti: Corona yasababisha idadi ya watu wanaopima virusi vya Ukimwi kushuka



Wataalamu wa afya na wanaharakati wa haki za wanaouguwa ugonjwa wa Ukosefu wa Kinga Mwilini wanasema janga la COVID-19 limezifanya juhudi za kupambana na UKIMWI kutengwa kando na malengo ya kuutokomeza kupuuzwa.


Ripoti mpya ya Shirika la Afya Ulimwenguni barani Ulaya (WHO Europe) iliyochapishwa mjini Geneva siku ya Jumanne (1 Disemba) ilisema janga la virusi vya corona limesababisha idadi ya watu wanaokwenda kupima virusi vya UKIMWI (VVU) kushuka kwa kasi, jambo linaloongeza uwezekano wa maambukizo mapya kusambaa na kupelekea watu wengi zaidi kuuguwa ugonjwa huo hatari.

“Watu waliokwishaambukizwa virusi vya UKIMWI na ambao hawatibiwi wana hatari zaidi ya kuambukizwa virusi vya corona na kuvisambaza kwa wengine”, ilisema ripoti hiyo iliyochapishwa kwa ushirikiano wa WHO Europe na Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Maradhi ya Ulaya, ECDC.

“Hii ni hali ya kutisha inapozingatiwa kwamba kwa muongo mzima uliopiza, maambukizo mapya ya VVU yamekuwa yakiongezeka kwenye eneo la Ulaya.” Ilisema sehemu moja ya ripoti hiyo iliyochapishwa kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani.


 
Uhusiano baina ya UKIMWI na COVID-19

HIV Virus, Aids, HDRI Bild, Mikroskopische AufnahmeTaswira ya virusi vya UKIMWI.
Kwa mujibu wa wataalamu walioshiriki kuandaa ripoti hiyo, kusambaa kwa UKIMWI kuna athari za moja kwa moja kwenye usambaaji wa maradhi mengine.

Baadhi wa wanasayansi wanaamini kuwa aina mpya ya kirusi cha Omicron kimetokana na mgonjwa wa VVU, kwani mtu mwenye VVU na akawa amepatiwa matibabu ya kiwango cha chini anaweza kuwa na mfumo wa kinga usio na uwezo, na hivyo kuufanya mwili wake kuwa mahala ambapo kirusi kinaweza haraka sana kujibadilisha sura zake mara kadhaa ndani ya wiki chache.

Ripoti hiyo inazungumzia pia usambazaji wa chanjo za corona usio na usawa unaomaanisha kwamba eneo la kusini mwa Afrika, ambalo lina idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, ndilo pia lilipokea chanjo chache zaidi.


Hali ya UKIMWI barani Ulaya

Winnie ByanyimaMkurugenzi wa Shirika la Kupambana na UKIMWI la Umoja wa Mataifa (UNAIDS), Winnie Byanyima.
Barani Ulaya, idadi ya maambukizo mapya ya VVU inapanda kwa asilimia 24, kwa mujibu wa mashirika hayo mawili ya afya. Eneo lililofanyiwa utafiti linajumuisha mataifa 53, zikiwemo Israel, Urusi, Uturuki na Turkeminstan, ambapo ripoti inasema kuna idadi kubwa ya watu walioambukizwa Ukimwi bila kujijuwa na ambao bado hawajakwenda kupima.

Kufikia mwaka jana 2020, katika mataifa 27 wa Umoja wa Ulaya, pamoja na Iceland, Liechtenstein na Norway, kulikuwa tayari na watu 14,971 walioripotiwa kuambikizwa VVU, ambapo kwenye eneo zima la Ulaya, idadi ya wanaoishi na virusi hivyo ni 104,765.

Utafiti uliofanywa na mashirika hayo mawili ya afya umebaini kuwa kwenye mataifa mengi ya Ulaya Magharibi, maambukizo ya virusi vya UKIMWI husambazwa kupitia kujamiiana wanaume kwa wanaume bila kutumia kinga.

Katika mataifa ya Ulaya Mashariki, maambukizo husambazwa kupitia uchomaji sindano kwa watumiaji wa madawa ya kulevya na pia ufanyaji mapenzi wa wake kwa waume usiozingatia kinga.


 
Hali ya UKIMWI ulimwenguni

AIDS-Bekämpfung, AngolaKampeni ya upimaji virusi vya UKIMWI nchini Angola.
Kiasi watu milioni 35 wameshafariki dunia kutokana na maradhi yanayoambatana na virusi vya UKIMWI tangu ugonjwa huo ugundulike mwaka 1984.

Umoja wa Mataifa ulikuwa umejiwekea lengo la kuutokomeza Ukimwi kufikia mwaka 2030, lakini ulijikuta haukuweza kutimiza hata malengo yake ya ndani kufikia mwaka jana 2020.

Kwa mujibu wa Shirika la Kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa (UNAIDS), endapo programu za matibabu zitaendelea kwa viwango vya mwaka 2019, kutakuwa na ongezeko la vifo milioni 7.7 kutokana na UKIMWI kufikia mwaka 2030.

Kukiwa na fedha zaidi, shirika hilo linakadiria linaweza kuokowa maisha ya watu milioni 4.6 katika hao.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post