Morrison Awashtua Mabosi Simba




UONGOZI wa Simba umepanga kukaa mezani na kiungo wake mshambuliaji Mghana, Bernard Morisson kwa ajili ya kumuongezea mkataba utakaondelea kumbakisha hapo.Morisson ni kati ya wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu ambaye alijiunga na timu hiyo msimu uliopita akitokea Yanga.

Mghana huyo juzi alionyesha kiwango kikubwa katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya nchini Zambia akifunga mabao mawili huku akipiga asisti kwa Mnyarwanda Meddie Kagere.


Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, uongozi umeridhishwa na kiwango cha kiungo huyo mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mhispania Franco Pablo naye amehusika kupendekeza kuongezewa mkataba kwa kiungo huyo baada ya kuvutiwa naye.Aliongeza kuwa kocha huyo hivi sasa amemhamisha kiungo huyo kutoka kiungo wa pembeni namba 11 na kucheza 10 nyuma ya straika kwa ajili ya kutengeneza mabao.

“Morisson ni kati ya wachezaji watakaongezewa mikataba mipya baada ya ule wa awali wa miaka miwili kumalizika mwishoni mwa msimu huu.“Ataongezewa mkataba kutokana na ubora aliokuwa nao, amekuwa akitoa mchango mkubwa katika timu na hilo amelithibitisha katika mchezo wetu wa shirikisho tuliocheza dhidi ya Red Arrows.“

Aliisaidia timu kufunga mabao mawili na kupiga asisti moja katika ushindi wa mabao 3-0 tulioupata, kingine zaidi amekuwa chaguo la kwanza la kocha Pablo baada ya kuvutiwa na kiwango chake,” alisema mtoa taarifa huyo.Akizungumzia hilo, Kaimu Ofisa Habari wa timu hiyo, Ally Shatry alisema: “Muda wa usajili bado, hivyo mapema kuzungumzia hilo, isitoshe Morisson bado mkataba haujamalizika bado mchezaji wa Simba.”


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post