Ripoti ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) imebainisha kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 haukuwa na mazingira sawa ya ushindani, jambo ambalo liliathiri ushiriki wa vyama vya upinzani.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana, imeandaliwa na Redet chini ya Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) baada ya kuangalia uchaguzi uliopita katika mikoa yote wakiwa na waangalizi 2,353.
Akizungumzia yaliyojiri kwenye uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Redet, Profesa Rwekaza Mukandala alibainisha mambo mbalimbali yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo, ikiwamo kukosekana kwa mazingira sawa ya ushindani.
“Vyama vya upinzani havikufanya vizuri katika uchaguzi uliopita na pia uwanja wa ushindani haukuwa linganifu, haukuwa sawa, kwa hiyo kwa kiasi fulani iliathiri ushindani na ushiriki wa vyama vya upinzani,” alisema Profesa Mukandala.
Profesa Mukandala alisema ushindani unategemea nyezo au rasilimali za kuwezesha kushindana, hivyo katika uchaguzi uliopita, vyama vya upinzani havikuwa na rasilimali za kutosha.
“Katika uchaguzi wa mwaka 2015, kulikuwa na mabango ya wagombea wa vyama vingine, Lowassa alikuwepo, Dk Magufuli pia…walikuwa wanakwenda sambamba lakini kwa uchaguzi wa mwaka jana kulikuwa hakuna mabango ya wagombea wa upinzani.
“Hii ni kwa sababu ya rasilimali ndiyo ilikuwa kikwazo, hawakuwa na uwezo wa fedha za kuweka hayo mabango ili yaonekane, kuwa na vipeperushi. Wagombea wengi hawakufanya mikutano ya kampeni, walikuwa wanasubiri siku za mwisho au wakati mgombea urais anapita,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa Redet alisema huko zilichukuliwa hatua kadhaa za kuhakikisha kwamba vyama vinapata ruzuku ambayo inaviwezesha kuzitumia katika uchaguzi, lakini katika uchaguzi uliopita, hilo halikuzaa matunda.
Alisema watu wengi walijitokeza kujiandikisha kupiga kura lakini siku ya uchaguzi, watu wengi hawakwenda kupiga kura. Alisema sababu za watu kutokwenda kupiga kura zinatakiwa zifanyiwe tafiti zaidi kujua kilichosababisha.
Profesa Mukandala alibainisha kwamba katika hatua mbalimbali za kupiga kura, vitendo vya rushwa vilishamiri, hasa katika kupata wagombea ndani ya vyama, alishauri vyama vihakikishe kwamba mchakato wao wa kupata wagombea unakuwa huru na wa haki.
Kuhusu suala la wagombea kuenguliwa kwa kukosea kujaza fomu za uchaguzi, Profesa Mukandala alisema jambo hilo ni tata kwa sababu kwa mujibu wa Katiba, kigezo kikuu cha mtu kugombea nafasi yoyote ni awe raia wa Tanzania.
“Vitu vingine kwamba aliweka ‘a’ badala ya ‘e’ iwe ndiyo sababu ya kumuengua, kwa kweli hiyo inatia shaka na huko katika chaguzi zote zilizopita hayo yalikuwepo…huko mbele tunakokwenda, watu wasienguliwe kwa sababu tu kakosea tarehe, tufuate katiba inavyosema,” alisema.
Awali akifungua mkutano huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Utafiti, Profesa Bernadetha Kilian alisema vyuo vikuu ni wadau muhimu wa kufuatilia kinachoendelea katika jamii, hivyo walishiriki katika kuangalia uchaguzi huo kama ilivyo utamaduni wao.
Alisema chuo kiliiwezesha Redet kutekeleza majukumu yake ya msingi katika uchaguzi huo na kwamba majukumu yake hayakuishia hapo, bali kuwawezesha wanawake pia kushiriki kwenye demokrasia kwa kuwapatia mafunzo maalumu.
“Ripoti za Redet na Temco zinawapatia wanafunzi ujuzi na rejea za kusoma wakati wa masomo yao. Tunazishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ZEC kwa ushirikiano wao,” alisema Profesa Kilian.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TLP, Richard Lyimo alisema ni muhimu kwa vyama vya siasa navyo kushirikishwa katika uandaaji wa ripoti hiyo ili vifahamu kilichokuwa kikiendelea majimboni na kupokea ushauri.
“Ningefurahi kuona kwamba hata sisi wadau wa siasa tunashirikishwa katika uandaaji wa ripoti hii na kupata ushauri wa moja kwa moja,” alisema Lyimo. Hata hivyo, Profesa Mukandala alimweleza kwamba hawawezi kuvishirikisha vyama vya siasa kwa sababu ripoti hiyo ni ya uangalizi wao.
Naye Mhadhiri wa Udsm, Dk Audax Kweyamba alisema ripoti imebainisha mambo ya msingi ambayo yanaonekana katika uchaguzi uliopita na jitihada zinahitajika kuhakikisha kwamba mapendekezo yaliyotolewa yanafanyiwa kazi ili uchaguzi ujao uwe bora zaidi.
Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa, Athuman Ismail alisema ripoti hiyo ya Redet itaongeza mjadala kwenye jamii na watu wanaweza kuzungumza kwa uwazi zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa siku za nyuma.
“Wengi wetu tunajua kuwa wapinzani walibanwa mbavu na mabavu yalitumika, hivyo leo hii huwezi kusema uchaguzi ulikuwa huru na haki,” alisema.
Itakumbukwa pia mgombea wa urais wa Chadema, Tundu Lissu alipinga matokeo yaliyompa ushindi hayati Magufuli, akidai yaligubikwa na udanganyifu.
Post a Comment