JARIBU kuvaa viatu vya mchezaji anayeitwa Heritier Makambo. Maisha lazima yatakuwa magumu kwake. Kitu pekee ambacho unaweza kumsifu ni uwezo wake wa kukaa kimya na kutolalamika kuhusu kile kinachomtokea Jangwani. Bado hajalalamika kwa waandishi wa habari.
Aliondoka Yanga kama shujaa miaka mitatu iliyopita. Amerudi Yanga kama shujaa. Hata hivyo nyota yake inafifia. Sidhani kama ni kwa sababu yake mwenyewe. Labda inawezekana kwa sababu ya kocha wake, Mohamed Nabi.
Filamu ilianza pale ambapo Yanga walikuwa sokoni kusaka washambuliaji wawili wakali wa kigeni baada ya kufeli kwa Michael Sarpong na Fiston Abdourazak. Kocha Nabi hakumtaka Makambo na wala hakuwa anamfahamu.
Akili ya Nabi ilikuwa kwa mshambuliaji mwingine wa kimataifa wa Congo, Jean-Marc Makusu. Nabi alikuwa analazimisha viongozi wa Yanga wamchukue Makusu na sio Makambo. Nabi alionyeshwa mikanda ya Makambo na jinsi ambavyo aliifanyia Yanga mambo makubwa lakini Nabi akagoma.
Viongozi wa Yanga nao wakamgomea kumchukua Makusu kwa madai kwamba staa huyo wa zamani wa AS Vita na Orlando Pirates alikuwa hajacheza soka kwa msimu mzima. Wakati huo huo viongozi wa Yanga licha ya kumkubali Makambo lakini pia walikuwa wakipokea shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki na wanachama kumrudisha Makambo.
Mchezaji ambaye jina lake lilikuwa limepita kwa pande zote mbili alikuwa Fiston Mayele. Mabosi wa Yanga walimtaka Mayele na Nabi pia alimtaka Mayele. Maisha yakawa rahisi kwa Mayele kuanzia siku yake ya kwanza Yanga.
Ndani ya akili ya Nabi nadhani Mayele hana mpinzani wa nafasi yake, labda kama angempata Makusu nadhani kungekuwa na mchuano mkubwa wa nafasi kati ya Makusu na Mayele lakini kwa hali ilivyo sasa maisha yamekuwa magumu kwa Makambo.
Bahati mbaya zaidi ni kwamba Mayele mwenyewe anatupia mabao kila uchao. Ni jambo zuri kwa timu lakini linakuwa jambo baya kwa Makambo. Kwanza kabisa mashabiki na wanachama wa Yanga wanajikuta wamemsahau Makambo ambaye anaoza kwenye benchi.
Wakati mwingine mashabiki wetu ni chachu kubwa kwa mabadiliko ya kikosi kama ambavyo majuzi mashabiki wa Simba walikuwa wameshinikiza kiungo wao, Ibrahim Ajibu arudishwe uwanjani katika pambano dhidi ya Namungo. Hii ilitokana na timu kutokuwa sawa.
Lakini kwa hali ilivyo sasa mashabiki wa Yanga hawawezi kuweka shinikizo la Makambo kupangwa wakati timu inashinda na Mayele anafunga. Matokeo yake ukikusanya dakika zote ambazo Makambo amecheza tangu ligi ianze haziwezi kufika hata 120.
Hili ni tatizo jingine kwa Nabi. Inawezekana kwamba Mayele amekuwa akifanya vizuri lakini hata hivyo anampa Makambo dakika chache zaidi. Matokeo yake ubora wa Makambo unazidi kupungua hata kwa hizo dakika anazoingia. Dakika anazoingia anashindwa kabisa kuthibitisha ubora wake kwa sababu hazimtoshi.
Kule kwa watani wao maisha ni tofauti. Leo anaweza kuanza John Bocco kisha Meddie Kagere akaingia dakika ya 70. Kesho anaweza kuanza Kagere kisha Chris Mugalu akaingia dakika ya 70. Kuna mzunguko mzuri (rotation) ambao unawapa washambuliaji wote nafasi ya kuwa fiti kadri msimu unavyosonga mbele.
Nabi anapolishindwa hili anatengeneza pengo kubwa kati ya Mayele na Makambo. Mbaya zaidi kunakuwa na pengo kubwa pia kati ya Mayele na mshambuliaji wa tatu wa timu hiyo, Yusuf Athuman ambaye naye ana dakika chache uwanjani.
Mayele na Makambo ni wachezaji wenye sifa tofauti uwanjani ingawa wote ni wazuri katika kuziona nyavu. Nadhani kinachomkosha Nabi kwa Mayele ni uwezo wake wa kujishikirisha zaidi na mechi achilia mbali kufunga.
Mfano mzuri ni bao alilofunga dhidi ya Mbeya Kwanza. Muvu ya bao lenyewe ilianzia kwake kabla hajaurudisha mpira kwa Saido Ntibanzokiza ambaye alimpasia Fey Toto kisha akampasia tena Mayele aliyefunga.
Hata hivyo, licha ya ubora huu wa Mayele lakini Makambo bado anastahili nafasi ya kucheza dakika nyingi uwanjani kwa sababu Yanga ya leo inatengeneza nafasi nyingi uwanjani. Kama aliweza kufunga mabao mengi katika kikosi cha kina Ajibu atashindwaje leo akiwa amezungukwa na mafundi lukuki kila upande wa uwanja?
Ujio wake wa pili una mabao mawili ambayo yote amefunga katika mechi za kirafiki. Kama Nabi akiendelea kumuamini na kumpatia dakika nyingi huenda akawa fiti zaidi na akamsaidia mbele ya safari tofauti na sasa anavyotengeneza pengo kubwa baina yao.
Kitu kibaya ambacho kinaweza kutokea kwa Makambo kwa sasa ni kama Yanga wakiamua kwenda sokoni na kununua mshambuliaji mpya katika dirisha dogo lijalo mwezi ujao. Nafahamu kwamba wao kama ilivyo kwa watani wao wana mipango hiyo. Timu hizi huwa hazina raha kama hazijasajili wachezaji wa kigeni katika dirisha lolote lile.
Nadhani Yanga watamsajili mshambuliaji ambaye moja kwa moja atakwenda kuwa chaguo la pili na kumfanya Makambo awe chaguo la tatu huku kijana wetu Yusuf akiangukia kuwa chaguo la nne. Huu ndio ukweli mchungu ambao mwisho wa msimu unaweza kumfanya Makambo atafute chimbo jipya.
Kilichomuondoa Horoya kilikuwa hiki hiki kitendo cha kuangukia kuwa chaguo la pili katika nafasi ya ushambuliaji. Bahati mbaya amejikuta katika mtego ule ule akiwa na timu yake ya zamani. Wakati anaondoka kumbuka kwamba alikuwa mshambuliaji chaguo namba moja.
Nini kifanyike? Makambo aendelee kujifua tu na aendelee kuwa kama alivyo. Awe mkimya. Mara nyingi wachezaji wa kulipwa huwa wanajibu mapigo wakipewa nafasi ya kuonyesha ubora wao uwanjani.
Post a Comment