YANGA inazidi kuwa tishio msimu huu kutokana na rekodi zake ikiwa tayari imekusanya pointi 12 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku watani zao, Simba wakiwa nazo nane.
Ukiangalia rekodi za msimu uliopita katika mechi nne za kwanza za Ligi Kuu Bara, kisha ukalinganisha na za msimu huu, ni wazi Yanga wanakimbiza ile mbaya kwa upande wa pointi, huku Simba wakizisaka rekodi hizo kwa tochi.
Msimu uliopita baada ya mechi nne za kwanza, timu hizo kila moja ilikuwa imekusanya pointi kumi kutokana na kushinda mechi tatu na sare moja, lakini msimu huu, Yanga imeongeza mbili ikishinda zote nne, Simba imepungukiwa na mbili baada ya kushinda mbili na sare mbili.
Katika mechi nne za kwanza msimu uliopita, matokeo ya Yanga yalikuwa hivi; Yanga 1-1 Prisons, Yanga 1-0 Mbeya City, Kagera Sugar 0-1 Yanga na Mtibwa Sugar 0-1 Yanga.
Kwa upande wa Simba, ilikuwa hivi; Ihefu 1-2 Simba, Mtibwa Sugar 1-1 Simba, Simba 4-0 Biashara United na Simba 3-0 Gwambina.
Rekodi za msimu huu wa 2021/22 upande wa Yanga zipo hivi; Kagera Sugar 0-1 Yanga, Yanga 1-0 Geita Gold, KMC 0-2 Yanga na Yanga 2-0 Azam.Simba wao wamepata matokeo ya aina hii; Biashara United 0-0 Simba, Dodoma Jiji 0-1 Simba, Simba 1-0 Polisi Tanzania na Simba 0-0 Coastal Union.
Mbali na rekodi hizo za pointi, lakini Yanga imeendelea kujiimarisha zaidi kwenye safu yake ya ulinzi ambapo haijaruhusu bao, huku ikifunga mabao sita na kukusanya clean sheet nne.
Msimu uliopita, iliruhusu bao moja na kufunga manne, ikiwa na clean sheet tatu katika mechi nne za kwanza.Simba wenyewe msimu uliopita katika mechi nne za kwanza, ilikuwa na clean sheet mbili, ikifunga mabao kumi na kuruhusu mawili. Msimu huu, ina clean sheet nne, imefunga mabao mawili.
STORI: LEEN ESSAU, Dar
Post a Comment