SIO ZENGWE: Somo tulilopata sakata la Morrison, Yanga



Si mara ya kwanza nasema hivi; ni kawaida yetu kutojifunza kwa tukio moja. Likipita limepita haliachi somo lolote kwetu.

Lakini walioendelea huchambua kila tukio na kulifanyia kazi ndio maana leo wana mifumo mizuri ya kufanyia kazi kwa kuwa walipata somo kutokana na tukio fulani. Usalama wa viwanjani unaoonekana leo England ulitokana na kufanyia kazi ripoti ya Taylor iliyohusu kiini cha janga la Hilsborough wakati mashabiki 95 wa Liverpool walipofariki Aprili mwak 1989.

Mchezaji kuwa huru kwenda popote bure anapomaliza mkataba wake ulitokana na juhudi za Jean-Marc Bosman, aliyepigania haki hiyo Mahakama ya Ulaya kuanzia mwaka 1990 akipambana na Chama cha Soka cha Ubelgiji baada ya klabu yake ya RFC Liege kumzuia kuhamia Dunkerque ya Ufaransa iliyoshindwa kufikia dau lililowekwa.

Hukumu iliyotoka mwaka 1995 na ndiyo iliyobadilisha maisha ya wanasoka Ulaya. Hukumu iliwaruhusu wachezaji kuanza mazungumzo na klabu mpya anayotaka kwenda katika kipindi cha miezi sita ya mwisho wa mkataba wake na klabu anayochezea.


 
Kwa hiyo, wale wanaoona hukumu ya Mahakama ya Usuluhishi wa Kimichezo (CAS) dhidi ya madai ya Yanga kuhusu uhalali wa mkataba wa Bernard Morrisson, bado wana mawazo mgando yasiyojifunza chochote kutokana na tukio moja.

Kwa kiwango fulani, baada ya takriban miaka miwili uamuzi wa shauri hilo kutolewa, kuna siasa ya kuepuka madhara ya kufuata haki imechukua mkondo. Ni vizuri kwamba uamuzi huo umekuwa upande wa Morrison, lakini naamini kuwa kama Yanga ingeshinda, kungekuwa na vurugu kubwa kwenye ligi yetu. Kama ingeamuliwa kuwa mkataba wa Morrison Yanga ulikuwa halali, maana yake hakuwa halali kuichezea Simba na hivyo mechi zote alizocheza msimu uliopita na huu zisingetambuliwa na matokeo kubatilishwa.

Hapo ingekuwaje?

Moto wa vyama vya michezo kutaka mashauri yake yasiende mahakama za kiraia siku zote ni kutaka masuala yake yafanyiwe maamuzi kulingana na utashi wa kimichezo. Ingekuwa katika mahakama ya kiraia, upande mmoja ungeweza kuwasilisha ombi la amri ya kumzuia kucheza hadi shauri kuu liishe; yaani asingecheza mwaka jana na mwaka huu hadi wiki iliyopita.


Lakini kimichezo na kuua kipaji na ndio maana wanamichezo wakataka wawe na vyombo vyao vya maamuzi ambavyo vinazingatia utashi wa michezo na hivyo kutovuruga au kuua vipaji vya wanamichezo.

Kama CAS imeshaamua, inawezekana hakuna hatua zaidi, lakini hilo linamaanisha nini?

Hadi Yanga inachukua uamuzi wa kwenda CAS, haikuwa imeridhika na uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, ikisema kuwa chombo hicho kilifanya uamuzi wa suala ambalo halikuwa mbele yake; kuamua kuhusu dosari za mkataba badala ya hoja kuu ya kuwepo au kutokuwepo kwa mkataba.

Maana yake ni kwamba kuna umuhimu sana wa kuimarisha utendaji wa vyombo vyetu vya maamuzi na kuvipa uhuru ambao hautasumbua katika kufikia maamuzi. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inaundwa na watu gani ambao wanaweza kuwa huru katika kufanya maamuzi?


 
Mmoja wa wanakamati alikuwa Zacharia Hanspope, mwenyekiti wa muda mrefu wa Kamati ya Usajili ya Simba. Mwingine ni Ulisaje, anayejulikana kuwa ni Yanga. Wajumbe wengine ni nani ambao ni lazima idadi yao iwe watano, maana yake ikifikia kupiga kura lazima kuwe na mshindi. Hao wanaoweza kuwa huru wanapatikanaje?

Kwa hiyo, kuna haja ya kukuna kichwa kutengeneza kanuni zitakazowezesha kupata wajumbe ambao wanaweka mbele maslahi ya mpira kuliko ushabiki.

Ni dhahiri kuwa wanasheria, ambao ni muhimu kwenye kamati hiyo, waliojijengea heshima katika kazi zao, hawawezi kujishushia hadhi kwa kufanya maamuzi ya upendeleo wakijua kabisa kuwa kwa jicho la sharia wataaibika.

Pia, ni muhimu kuwe na mfumo wa kuhakikisha uamuzi wa vyombo hivyo kama Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, unakatiwa rufaa kwanza ndani kabla ya shauri kwenda vyombo vya haki vya nje. Na chombo kitakachokuwa kinasikiliza rufaa ni lazima kiwe na heshima hiyo ya kuaminika mbele ya jamii kwa kufanya maamuzi ya haki yasiyo na dosari hata kidogo.


Pamoja na kuaminiwa kwa kupewa dhamana hiyo duniani, CAS imekuwa ikilalamikiwa kutokana na kutokuwa na uwazi, uteuzi wa wasuluhishi kuwa na maswali—kati ya wasuluhishi 400 walio katika orodha yao, ni asilimia 30 tu ndio hutumika--, maamuzi ya wasuluhishi kuhaririwa na mkurugenzi mkuu wa CAS kwa jinsi apendavyo na nguvu ya ICAS, Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) na vyombo vingine katika kushawishi maamuzi na wajumbe wengi kuwa viongozi wa mashirikisho na vyombo vingine.

Ili kuepuka kufika katika dosari hizo, ni muhimu kuwa na vyombo vyetu imara vya haki ili tumalizane humuhumu ndani.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post