Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla amewaonya watendaji wanaowachia wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga kurudi maeneo yaliyokatazwa.
Makalla aneyasema hayo leo Jumatatu Novemba 22, 2021 kwenye uzinduzi wa mkakati wa usafi na uhifadhi mazingira wa mkoa huo uliopewa jina la 'Safisha Pendezesha Dar es Salaam' baada ya kufanikisha kuwondoa wafanyabiashara hao maeneo yasiyo rasmi.
Amesema katika hilo, watendaji wanapaswa kuelewa kuwa kuondolewa kwa wamachinga ni maagizo ya Rais hivyo kila mmoja ana wajibu wa kilisimamia hilo badala ya kuona ni kazi ya Mkuu wa Mkoa.
Amesema mpaka wamefikia hatua ya kuja na mkakati wa kufanya usafi ni kwamba vikwazo vilivyokuwepo wamefanikiwa kuviondoa ambavyo mojawapo ni ya wamachinga.
"Nashukuru shughuli ya kuwaondoa wamachinga imeenda vizuri, kwani mpaka sasa tumefanikiwa kwa asilimia 90, sasa kuwaaacha warudi tena ina maana wewe mtendaji hujatimiza wajibu wako, hivyo hili sitalifumbia macho na ndio maana tumesainishana hadi mikataba hapa, tutaanzia hapo,"amesema Makalla.
Ametolea mfano kuwepo kwa uzembe kwa Kata ya Wazo na Mwenge, kuwa kuna baadhi ya watendaji wamekuwa wakiruhusu wafanyabashara hao kurudi barabarani na kuwapa kichwa kwamba hawatafanywa lolote jambo ambalo sio sahihi na kuonya wasithubutu kufanya hivyo kwa kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Makalla amezitaka taasisi ambazo wamachinga waliondolewa mbele ya majengo yao kuanza kuzilinda maeneo hayo wenyewe kwa kuwa kama mkoa wameshafanya kazi kubwa ya kuwasidia kuwaondoa.
Post a Comment