Profesa Jay akiri kuacha kazi kisa muziki
MSANII mkongwe wa Bongo fleva, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ amesema aliacha kazi kwa ajili ya muziki ili apate muda wa kufanya muziki wake.
Akizungumza na gazeti hili, Profesa Jay alikiri kuwa ilifika wakati akafanya maamuzi magumu ya kuacha kazi katika kampuni ya Mobitel (wakati huo) na sasa inaitwa Tigo ili awe huru kufanya muziki wake na kufanya shoo zake mikoani na maeneo mengine.
“Nilikuwa nakosa muda wa kufanya muziki, wakati huo nafanya kazi Mobitel Mkoa wa Tanga, nikaamua kuacha baada ya kuona kipato nilichokuwa nikipata kwa mwezi hakikulingana na mkwanja niliokuwa nikitengeneza kupitia muziki,” alisema.
Baadhi ya watu walinishangaa kuona naacha kazi kwa sababu ya muziki ambao kwa wakati huo ulikuwa unaonekana kama ni uhuni.
“Nilianza kazi mwaka 1998 na mwaka 2005 nikaamua kuacha baada ya kuona sina muda wa kufanya shoo kwani mwaka 2000 nilitoa wimbo wa Chemsha Bongo ambao ulikuwa unafanya vizuri hivyo nilikuwa naalikwa natoroka kazini lakini siwezi kurudi kwa wakati,” alisema.
Alisema Chemsha Bongo uliibadilisha tasnia ya muziki, taswira na mitazamo ya watu kuanza kuamini muziki na wazazi wakawaruhusu watoto wao kuingia kwenye tasnia hiyo tofauti na hapo awali ambapo Bongo fleva ilionekana kama muziki wa kihuni.
Post a Comment