Mawazo Yangu ya Kina Juu ya Sakata la Diamond Platnumz na Harmonize..Nani Mkosaji?

Mambo yanakwenda kasi sana, joto linazidi kukimbiza huku jua likichoma kishenzi. Wakati tukifikiria ni kwa namna gani tunaweza kusurvive huku maji na umeme vikiwa shida, wasanii nao wanaibuka na mambo yao, yaani ni shida juu ya shida.

Haya! Wengi mmeniambia nije na makala kuhusu jambo hilo, basi niseme ninakuja na hii makala, ila kabla ya kuendelea, weka uteam pembeni kwanza, tuzungumzie mambo halisi.

Mimi sina timu, huwa ninazungumza kitu ambacho ni cha kweli, kile kilichokuwa kwenye mtazamo wangu, kubwa zaidi, huwa si mpenzi wa miziki ya Bongo fleva, hata simu yangu, huwezi kukuta ngoma za hapa Bongo.

Lakini kwenye yote, acha nijaribu kuelezea kile nilichokiona tangu siku ya kwanza Harmonize anapoondoka WCB mpaka leo, nitajaribu kufafanua ninayoyaona, kama una yako, basi na wewe kaandae makala tuje kusoma.

MKATABA WA 40%

Nianze na suala la mkataba. Kwanza kitu cha kwanza tujue unapokuwa huna pesa, una maisha magumu, ukiletewa mkataba wowote ule ambao unaonyesha utakuwa unaingiza pesa ni lazima utausaini kwa sababu usipousaini, inamaanisha unakubaliana na maisha ya dhiki unayoishi.

Leo nikisema ninahitaji waigizaji kwenye filamu yangu, halafu nikisema bwana mimi sina hela ya kumlipa msanii, ila ukifanya kazi na mimi, utapata jina na kuitwa kwenye muvi za watu wengine, utaacha nafasi hiyo kwa sababu hutolipwa? Je, utaendelea kukaa kwenye maisha hayo na kuachana na opportunity ambayo itakufanya kujulikana?

Kwenye hili! Kwanza tusimlaumu Harmonize kwamba kwa nini amesaini mkataba wa kulipwa asilimia 40 kwa sababu naamini hata ungekuwa wewe, kwa maisha ya dhiki, halafu unajua nikifanya kazi na Mondi, nitajulikana na kutengeneza pesa, kwa nini usikubali?


Kampuni nyingi za Tanzania zina mikataba mibovu na tunaiingia kwa sababu tuna shida ya pesa, tupo kwenye maisha ya kimasikini sana, unakubali kusaini mikataba mibovu kwa sababu unataka pesa, ama umaarufu ili baadaye utusue.


Unapoingia kwenye mikataba hiyo, unaona kabisa unanyonywa, ila huna ujanja, kuna kitu unakitafuta lakini moyo wako unasema siku moja nitaondoka tu, nikishapata pesa za kutosha nasepa.


Hilo ndilo wamekuwa wakilisema hata wajasiriamali, unapotaka kuanzisha biashara yako, kwanza anza kuajiriwa, upate pesa kisha ondoka ukaanzishe biashara yako, ndivyo ilivyokuwa kwa Harmonize.

Asingeweza kukaa WCB milele, ilikuwa ni lazima siku moja aondoke. Ukishapata pesa na umaarufu uliokuwa unautaka, sasa unasema huu ndiyo muda wa kuondoka, unaondoka zako, kuna watu wengi wamefanya hivyo, yeye si wa kwanza.

Kosa kubwa wanalofanya WCB ni aina ya mikataba wanayoingia na wasanii, msanii akiondoka, akilipia pesa, imekula kwao ila si kama lebo nyingi za Marekani.

Leo hii Drake, Nicki Minaj hawapo Young Money, ila kwenye kila pesa wanayotengeneza huko walipo, kuna asilimia inaingia kwenye lebo hiyo na maisha yanasonga.

Suala la Harmonize kuingia mkataba wa aina hiyo, simlaumu kwa sababu hata wewe unayesoma hapa, huko kazini kwako umeingia mkataba wa aina hii hii, hujilaumu wewe, unamlaumu Harmonize.

Kijana wa Kitanzania anapotaka kutafuta jina ama pesa, anakuwa tayari kufanya jambo lolote lile. Nilipokea meseji nyingi tu, mtu anakwambia “Bro! Natamani kuigiza, nitaigiza hata bure.”

Unajua anamaanisha nini? Anachohitaji ni kutafuta jina, anaamini hapo baadaye atakuja kuwa na jina na atapiga pesa tu kwani akihitaji pesa sasa hivi, anaweza asizipate na ukawa mwisho wa ndoto zake.

Sasa mtu huyu akikubali kuigiza bure ama kwa malipo madogo, siku akipata jina na kutaka kuondoka, cha kwanza tutatakiwa kupitia mkataba wake, tufanye tulichokubaliana na tuache aondoke.

Maisha popote pale.

HARMONIZE VIJEMBE KWA MONDI

Harmonize aliondoka WCB na kilichofuata ni kutoa vijembe na matatizo yaliyokuwepo hapo. Kuna wengi walisema kwa nini asingesema akiwa hapo? Kama wewe unajiuliza swali hilo, jishike kifuani na sema mimi ni mjinga sana.

Kuna wachezaji wengi wa mpira wakiwa timu fulani, hawazungumzi mbovu, ila wakiondoka ndipo utasikia ile timu mbaya sana, kocha magumashi na mengine mengi.

Ukiwa kwenye nyumba mbaya, husemi kwa watu kwamba ni mbaya, utataka uondoke halafu ndiyo useme ilikuwa nyumba mbaya.

Leo umeoa, huwaambii watu kama mkeo ni malaya, unasubiri umuache ndiyo uanze kusema yule mwanamke alikuwa malaya, halafu hajui kupika, kikojozi na kitandani gogo. Kwa nini usiseme wakati akiwa ndani?

Madhaifu ya sehemu tunayasema tukishaondoka sehemu hiyo.

Suala la Harminize kumpiga vijembe Mondi ni kawaida kila kona. Bado ana hasira, labda kwa yale aliyowahi kutendewa ambayo aliona hayafai, taswira ikimjia, anakuwa na hasira na kujikuta ameropoka hili na lile.

Mtu akiondoka sehemu kwa vita, atahitaji kukaa muda mrefu mpaka akili yake kuja kukaa sawa.

HARMONIZE AMEKOSEA?

Jibu ni ndiyo! Wakati mwingine unapoondoka sehemu, achana na kila kitu, nenda kafanye mambo yako, achana na yaliyopita. Harmonize alishindwa kufanya mambo yake.

Alimkalia Diamond kooni, akaikalia WCB kooni, akawa anatoa vijembe kutwa. Nikahisi labda naye Diamond kwa kuwa amekuwa mkongwe angekaa kimya, ila cha ajabu naye akaanza kumrushia vijembe hasa kwenye nyimbo ambazo alishirikishwa, nikajua wote bado ni watoto ama kila mtu hataki kuonekana mpole kwa mwenzake.

MONDI AMEKOSEA?

Kuna msemo wa Kitanzania unasema ukigombana na mtu mmoja halafu ukasema ana matatizo, basi tunaweza kuamini kwamba kweli ana matatizo, ila ukigombana na watu watano, tutashindwa kukuelewa ukisema wana matatizo, tutakwambia kwamba wewe ndiye una matatizo.

Leo ukiniambia Mondi ana matatizo, nitakataa hilo, yeye hana matatizo bali watu waliomzunguka ndiyo wana matatizo. Namfahamu msela, nimekua naye mtaa mmoja, tangu kishuleshule mpaka alipoanza muziki japo sisi wengine tulikuwa bize na shule.

Jamaa ana uswahili kama sisi ila kuhusu roho mbaya, kwa mchizi hilo nakataa kwa kuwa tabia ni kama ngozi, huwa haijifichi, ningeliona hilo tangu kipindi kile alipokuwa akitoroka shule na kwenda kuimbaimba kila alipoona muziki ama kutafuta hela kwa kuuza nguo kwa kudandia Tandale sokoni.

Unapokuwa unakutana na watu ambao wanaweza kuibadilisha akili yako na kukupa nyingine kabisa. Ukiwapa nafasi, wanachukua maamuzi yao mabovu na kuwa yako, na wanafanya lolote lile ambalo mwisho wa siku litaonyesha taswira mbaya juu yako.

Kama ulifuatilia mwanzoni, vijembe vingi vya Harmonize havikuwa kwa Mondi moja kwa moja, alijua kabisa mchizi alikuwa mtu poa ila kuna mtu ambaye hakuwa poa, na ndiye aliyekuwa akimpiga vita sana.

Na ninadhani baada ya kuonekana hajibu kitu, ni kama akashinikizwa kujibu, naye ndipo alipoanza kujibu.

Kosa la Diamond ni kuanza kujibizana na Harmonize. Angekaa kimya tu, mtu umekwishamtoa, umemfanya kujulikana kupitia wewe, ana kitu gani cha kujimwambafai kwako? Wewe nyamaza tu, dunia itaendelea kujua kwamba bila wewe, yeye asingekuwepo hapo alipokuwa.

Kumjibu Harmonize ni jambo baya sana ambalo Diamond amelifanya, alitakiwa kuwa kimya tu, aendelee kufanya mishe zake kama kawaida kwa sababu siku zote huwezi kumfananisha yeye na Harmonize, bado ni kijana mdogo sana kwenye mafanikio ya muziki.

Kinyago umekichonga mwenyewe, kinakutishaje? Unakiogopea nini? Kama ningekuwa Mondi, nisingemjibu Harmonize ama kumpa kijembe kwenye wimbo wowote ule, ningewakataza Juma Lokole na Baba Levo kumuongelea Harmonize, yaani ningeachana naye mazima. Kumuongelea na kumtupia vijembe inaonyesha kabisa naye Mondi anatamani kusikika mitandaoni akibishana na Harmonize ambaye kiukweli ni mdogo mno kwake.

NI KWELI HARMONIZE AMEBADILIKA?

Bado najiuliza swali hilo. Nakumbuka kipindi cha nyuma wakati akiwa WCB, wakati huo nikiwa mwandishi wa habari. Hakuna kitu ambacho Harmonize anakikataa kama kumuona mtu akipiga picha na Diamond. Yaani alikuwa anakukazia ileile.

Harmonize alikuwa maana halisi ya mringaji, alijua kufanya kitu chochote kile usimfikie Diamond kwa lolote lile, hata ukiwa shabiki wake kwa namna gani, ila leo namuona si Harmonize yule, amekuwa mnyenyekevu, mpole na amekuwa na moyo wa kusaidia wengine, huwa ninajiuliza kutoka WCB kumembadilisha kuwa hivyo ama kule aliambiwa awe na maisha yale hata kuwabania watu kupiga picha na Mondi? Sijapata jibu.

KOVU LA HARMONIZE LITAMTESA MONDI MILELE

Harmonize alikuwa msanii wa Mondi, yaani yeye ndiye ambaye alimchukua yeye kama yeye, si kama hao wengine ambao ameletewa. Harmonize alikuwa kipenzi cha Mondi, aliaminiwa na kuonyeshwa chocho zote.

Kipindi kile Mondi alipokuwa akisafiri, alikuwa akiongozana na Harmonize kila kona, alimtambulisha kwa kila mtu, kwa kifupi alimwamini kwa kuwa alikuwa msanii wake, hakuletewa kama ilivyokuwa kwa hao wengine.

Ukiangalia kipindi hicho, Mondi alikuwa akisafiri sana na Harmonize kuliko hata Rayvanny, alijua kwamba huyu ni msanii wangu mimi, mrithi wangu, halafu ghafla tu, huyo mrithi akasepa zake. Kama ni kupigwa na kitu kizito kichwani, basi Harmonize amejua kumpiga nacho Mondi.

Suala la Harmonize litaendelea kumtesa, kama ni mzimu wake basi utaendelea kumtokea. Rich Mavoko ameondoka WCB lakini humsikii Mondi akimzungumzia, wengine watakuja na kuondoka, hatowazungumzia, ila kwa Harmonize, hatoweza kujishika hata kidogo.

Alitumia pesa na muda kwa ajili yake, alimwamini, akampa kila kitu ili dogo atusuea, kipindi kile akampa mpaka mademu wa kupiga nao skendo, mara katoka na Wolper, mara na huyu, yaani yote ilikuwa ni kumtengenezea jina dogo ili afuatiliwe, mwisho wa siku kilichotokea, kimemuumiza mno mno mno.

HIVI MMEMFIKIRIA RAYVANNY YUPO KWENYE HALI GANI?

Huyu amesahaulika. Jana baada ya kusikia mahojiano ya Harmonize na kuplay ile voice record, nikaanza kumfikiria Rayvanny yupo kwenye hali gani. Kuna jamaa mmoja mpenzi wa WCB aliweka video zikimuonyesha Rayvanny akiwa kwenye mahojiano kipindi cha nyuma akisema alihisi anarekodiwa na Harmonize, nikamuuliza jamaa maswali kadhaa.

Mtu ameondoka WCB kwa ugomvi mzito, leo anaongea na wewe, unajua kabisa unarekodiwa, je, ungeweza kumtemea shit bosi wako? Yaani mimi nimeondoka kwa ugomvi, halafu unaongea na mimi, unajua kabisa nakurekodi, je, ungeongea shit kwa bosi? Jibu ni hapana.

Rayvanny hakuwa akijua hilo ila baadaye akasanuka kwamba inawezekana yale mazungumzo yake na Harmonize yalikuwa yakirekodiwa, akaamua kujitetea mapema kabisa ili siku yatakapokuja kuwekwa hadharani basi tuseme jamaa alijua kama alikuwa akirekodiwa. Wakati mwingine inahitaji akili kubwa kucheza michezo ya kijanja.

CHUKI, HOFU VIMETAWALA BONGO

Kitu ambacho nakataa na nitaendelea kukataa ni pale mtu akiniambia kuna siku muziki wetu utasikika duniani kama ulivyo muziki wa Nigeria, hicho kitu sahau bro!

Sisi tumejaza chuki mioyoni mwetu, Watanzania hatupendani, unaweza kuzungumza na mtu vizuri, kumbe anakuchukia na hujui, anaziba baraka zako na hujui kabisa.

Wanamuziki wanachukiana wao kwa wao, mbaya zaidi kwa sasa wapo kimakundi, yaani kuna Team Mondi, Team Harmonize na Team Kiba, kwa staili hiyo tutafika vipi huko mbele? Hatuwezi.

Leo tutawaona wasanii wakigombea tuzo, bila aibu, nampigia kura msanii wa nje na kumuacha wa ndani, hiki ni kitu ambacho Wanigeria hawakifanyi, wanapoamua kusapotiana, wanasapotiana kwa asilimia mia moja.

Leo Burna Boy anakwenda Marekani kuperform, anawachukua maunderground wake anapaa nao kwenda huko, anawatambulisha jukwaani na ngoma zao zinapigwa, na hata kuperform, wanatangazana tu baadate tunasema huyu Burna Boy na Mondi, Mondi mkongwe, ila leo ukiuliza nani mwanamuziki mkubwa, utasema Burna ni mkubwa mara kumi ya Mondi.

Hatuwezi kufika mbele bila kusapotiana. Kwa kitendo cha Mondi kwenda Marekani bila kuwa na msanii yeyote yule ni kosa, analeta ubinafsi lakini simlaumu sana kwa kuwa yamekwishamtokea puani kwa Harmonize, alimuonyesha njia mwisho wa siku akaachwa kwenye mataa, wakati mwingine bora uonekane mbinafsi kuliko mjinga.

Kwa maelezo ya Harmo kipindi cha nyuma alisema kwamba ukienda Nigeria, ni vigumu sana kusikia klabu wakipiga ngoma za Tanzania, ila cha ajabu, sisi tunaongoza kupiga ngoma zao.

Niwaambie tu, ili muziki wetu ufike mbali, tusubiri hizi zama za Mondi, Kiba na Harmonize zipite, waje wengine wenye kiu ya kuwainua wengine kimataifa, kidogo tutaweza kusogea.

JPM ALIWEKEWA WAKATI MGUMU

Hayati JPM alikuwa kwenye wakati mgumu sana. Mondi na Harmonize walikuwa vijana wake, aliwapenda na kuwapamba wote wawili, mwisho wa siku akapokea simu kutoka kwa Harmonize na kuombwa msaada wa kitu ambacho Mondi hakuwa akikitaka bila shaka.

Kama mzazi, lazima utakuwa na wakati mgumu, hapo ni lazima umfurahishe mmoja na kumliza mmoja, ila alichokiangalia na kukifanya, ni hekima kama mtu mzima, simu yake moja kwa Waziri Mwakyembe ikamuweka Harmonize huru. Pongezi sana kwake kwa hekima zake.

Kuna kila sababu ya Harmonize kulia sana msibani mpaka kuchora tattoo ya Hayati JPM. Alimfanyia mambo mazuri likiwemo hilo, na kwa kile alichomfanyia, tattoo hiyo haitakiwi kufutwa mwilini mwake mpaka kifo chake. Bila yeye, inawezekana asingekuwa huru mpaka leo.

NB: Kweli Konde Jeshi, yaani amekaa na haya yote kwa miaka mitatu na wakati Manara alishindwa kukaa nayo hata kwa wiki moja tu.

By Chilojnr



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post