Davido Amwaga Shilingi Bilioni 1.4 Kwa Watoto Yatima..Ni zile Alizochangisha







Kupitia akaunti yake ya Instagram, msanii mahiri nchini Nigeria, David Adedeji Adeleke almaarufu Davido ametangaza kutoa msaada wa milioni 250 sawa na takribani shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kuwasaidia watoto yatima nchini Nigeria.

Staa huyo wa ngoma kibao kama Assurance, Fall na If ameandika kwamba siku chache zilizopita, aliamua kuomba fedha kwa mashabiki zake kama pongezi ya siku yake ya kuzaliwa ambayo huwa anaizimisha kila ifikapo Novemba 21 ya kila mwaka.

Anaeleza kwamba japokuwa alianzisha jambo hilo kama masihara mitandaoni, mwitikio alioupata umekuwa mkubwa kuliko maelezo ambapo ndani ya siku mbili tu, kiasi cha Naira milioni 200 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 1.1 zilichangwa kama pongezi kwake.

Amesema kutokana na wema mkubwa uliooneshwa kutoka kwa mashabiki zake, kwanza anawashukuru sana lakini pia ameamua kuongeza kiasi cha Naira milioni 50 na kufanya idadi ya fedha zote kuwa Naira milioni 250 ambazo zitagawiwa kwenye vituo vya kulelea watoto yatima nchini Nigeria pamoja na kuchangia katika mfuko wa Paroche Foundation.

Staa huyo aliyeimba na Chris Brown ngoma mbili za Blow My Mind na Shopping Spree ameeleza kwamba ili kuweka uwazi katika matumizi ya fedha hizo, amewateua watu watano kuunda kamati maalum inayojumuisha viongozi wa dini na watu mashuhuri, wakiongozwa na mwanamama Titi Adebayo ambayo ndiyo itakayoratibu mgao wa fedha hizo.

Amezidi kufunguka kwamba kamati hiyo itakaa chini na kuorodhesha idadi ya vituo vyote vya watoto yatima nchini humo na idadi ya watoto wanaolelewa pamoja na mahitaji yao yatima kisha fedha zitagawiwa kwenye vituo vyote kulingana na mahitaji ya watoto husika.

Amesema kutokana na mwitikio huo alioupata, anafikiria kufanya zoezi hilo liwe endelevu ambapo kila mwaka katika siku yake ya kuzaliwa, atakuwa akiwachangisha mashabiki zake na kwenda kutoa kwenye vituo vya watoto yatima na wenye uhitaji huku akihitimisha kwa msemo wa Kiingereza wa we rise by lifting others, akimaanisha tunanyanyuka kwa kuwainua wengine



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post