Boji: Mbwa anayetajwa kuwa 'abiria' mtiifu zaidi anayetumia usafiri wa umma




Siku hizi abiria katika mji wa Istanbul, Uturuki wanamtizama kiumbe hai ambaye amekuwa maarufu katika jamii hiyo. Kiumbe huyo ni mbwa wa mtaani, anayeitwa Boji, ambaye anapenda kusafiri kwa gari katika jiji kubwa zaidi la Uturuki.
Anasafiri kwa mabasi, treni na boti.

Hakuna anayejua jinsi alivyojifunza aina hiyo ya maisha ya kusafiri safiri kwa usafiri wa umma. Lakini dereva wa moja ya mabasi ya umeme katika mji huo alisema wanamfahamu Boji, na kwamba adabu na tabia yake wakati wa kuingia na kutoka kwenye gari lake inapaswa kuwa mfano kwa abiria wote ambao ni binadamu.

Boji amekuwa akivutia mioyo ya wakaazi wengi wa Istanbul mara kwa mara, na kuwafanya watu wengi kushangaa jinsi alivyozoea utamaduni wa safari kama hizo.

Aylin Erol, anayefanya kazi kwenye sekta ya usafiri wa reli mjini Istanbul, alisema baada ya kuona picha za mbwa huyo zimewekwa kwenye mitandao ya kijamii, waliamua kumuwekea kifaa maalumu ili kufuatilia harakati zake haswa.

Kwa mshangao wao, waligundua kuwa Boji hupita kwenye vituo angalau 29 vya treni kila siku, na safari zake kwa siku zinaweza kufikia umbali wa hadi kilometa 30 kwa siku. Katika jiji la Istanbul, ambalo lina boti mbili kwenye mwambao wa Ulaya na Asia, lina mfumo mgumu sana wa boti, lakini ni rahisi kwa Boji kusafiri.

Je Boji anapenda kusafiri?
Boji alionekana wakati mwingine baharini katika safari ya Visiwa vya Prince katika Bahari ya Marmara, ambayo iko nje kidogo ya Istanbul.

Umaarufu wa Boji unaokua unaenda sambamba na ukuaji wa akaunti yake ya Twitter.

Tangu kuzinduliwa kwa ukurasa wake wa twitter wenye jina @boji_ist zaidi ya watu 90,000 wametembelea kwa mwezi Septemba tu.

"Anajua anakokwenda, anajua pa kwenda," Aylin Erol, afisa wa uchukuzi alisema.

"Inaonekana anajua anachokifanya."

Ana kifaa kinachomfuatilia?
Boji alichomwa chanjo ili kumlinda yeye na wengine walio karibu naye.

Amewekewa kifaa cha sumaku kilichounganishwa kwenye programu maalumu ya simu ili kusaidia mamlaka kufuatilia hali yake ya afya.

Wafanyakazi wa usafiri huhakikisha anakula vizuri na kunywa maji vizuri. Serikali pia humfanyia uchunguzi wa mara kwa mara wa afya yake kupitia daktari wa mifugo.

Maelezo na video iliyowekwa chini ya jina la Boji inamuonyesha mbwa huyo akiwa na uzito wa kilo 42.

Ni mbwa maarufu kuwahi kutokea?
Kwa sababu sura yake imezoeleka, Boji sasa amekuwa akipokelewa na abiria wengi wanaomsalimu kwa upole, au kupiga naye picha 'selfie'.

Kwa mujibu wa taarifa za huduma za mifugo za Manispaa ya Istanbul, jiji hilo lina zaidi ya paka na mbwa 300,000, lakini baadhi ya watu wanaamini kuwa haya ni makadirio ya chini.

Mnyama huyu wa kipekee amekuwa kwenye midomo ya wakazi wengi wa Istanbul.

Katika miaka ya 1990, jiji hilo lilituma timu maalumu za kuwangamiza wanyama wanaozurura ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya paka na mbwa. Lengo lilikuwa kuondoa uwezekano wa kusambaza magonjwa kwa binadamu

Lakini baada ya watu kukosoa utaratibu huo, zoezi hilolilisimamishwa.

Kwa sasa maafisa wa manispaa badala ya kuwangamiza wamekuwa wakiwahudumia kwa kuwapa chanjo na kutibu matatizo yao kiafya.

Ni abiria mzuri?
Boji anazungumzwa vizuri sana huko Istanbul.

"Unaingia kwenye treni, ghafla, unamona Boji," Aylin Erol alisema.

"Unatabasamu tu na kufurahia wakati wako, kwa kweli, hivi ndivyo Boji anafanya kwa watu wa Instanbul. Inatukumbusha kwamba tunaweza kufurahia Istanbul huku tukiendelea harakati zetu," alisema Aylin Erol.

 



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post