Bei kubwa vifurushi vya data mwiba maendeleo ya kidigitali Tanzania
Wadau walia kila kona vifurushi kupanda maradufu tena kimya kimya
Tasnia ya habari Mitandaoni, elimu, Dini, Burudani waathirika pakubwa
Kutokana na kupanda maradufu kwa bei za vifurushi vya interneti nchini, huku GB 1 ya Data ikipatikana kwa zaidi ya dola 1.3 kumesababisha kupungua kwa kasi idadi ya watumiaji wa internet nchini hivyo kuathiri taasisi, mashirika na watumiaji binafsi wa interneti ambao hutumia huduma hiyo katika majukumu mbalimbali pamoja na burudani.
Aidha, kutokana na bei hizo kutokuwa rafiki kwa watumiaji wa huduma hiyo hasa mwananchi wa kawaida Taasisi na tasnia mbalimbali zimetajwa kuathirika kwa namna moja au nyingine
Tasnia ya habari za kidigitali
Watoa huduma za maudhui katika Tovuti na programu tumishi na mtandao wa YouTube na Blogs
wamelalamika kutokana na kushuka kwa kasi kwa watumiaji wa huduma zao
huku wakiiomba wizara na wadau husika kujadili na kulipatia mwarobaini
suala hili.
Ili kuendesha mitandao ya kijamii inatakiwa kutumia bando kila wakati ili kuendelea kuuhabarisha umma kuhusu habari na matukio mbalimbali hivyo gharama kubwa za vifurushi zimekuwa kikwazo kwa Bloggers & YouTubers.
Tasnia ya Burudani
Wasanii na watoaji maudhui ya burudani hasa kwa mtandao wa video wa YouTube
nao wamedai idadi ya wanaofuatilia kazi zao kushuka kwa kasi kwa siku
za karibuni, jambo ambalo wamedai kuathiri sana kipato chao. Vilevile
mitandao mbalimbali ya takwimu inaonesha kushuka kwa watumiaji wa
mtandao wa YouTube Tanzania kwa siku za karibuni.
Watumiaji Binafsi
Watumiaji mbalimbali wa internet Tanzania nao wameonesha kukerwa na
kupanda Mara kwa Mara kwa bei za vifurushi tena vinapandishwa kimya
kimya licha ya mamlaka kusema gharama zimeshuka huku wakidai uishaji wa
haraka kuliko kawaida wa vifurushi hivyo, vile vile wanakumbusha ahadi
za wadau na wizara kuahidi mara kadhaa kulishughulikia tatizo hilo na
kubakia ahadi hewa.
Pamoja na hayo, Bei hizi ambazo zimetajwa kutokuwa rafiki kwa watumiaji huenda zikazidi kuathiri mfumo mzima wa maendeleo ya kidigitali hasa kwa mashirika, taasisi, na makampuni kama vile huduma za kibenki za kidigitali, huduma za afya, elimu, na dini zinazopatikana kwa njia za kidigitali pamoja na tasnia ya michezo ya bahati nasibu ya mtandaoni.
Haki ya kupata taarifa, imeathiriwa
Kila mtu ana haki ya kupata taarifa, kwa miaka ya karibuni kutokana na
ukuaji wa maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano hata Serikali
imekuwa ikitoa taarifa zake kwa idara mbalimbali kwenda kwa wananchi
kwa njia ya mitandao, hii inahusisha hata Matangazo ya moja kwa moja ya
Uapisho wa viongozi, uzinduzi wa miradi na hotuba za viongozi kwa
wananchi ambao wapo maeneo tofauti tofauti. Kutokana na kupanda kwa
gharama za bando baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanakosa
haki ya kupata taarifa hizo kutokana na bando kupaa.
Hapo awali ilikuwa rahisi mtu kuweza kufatilia mubashara matangazo mubashara ya matukio ya kitaifa kupitia mtandaoni lakini hivi sasa wananchi wengi tunapata shida kuweza kuangalia hadi mwisho matangazo hayo kwani maranyingi kabla tukio halijaisha kifurushi cha data kinakuwa kimeshaisha, hivyo athari hizi si tu kwetu wananchi ila hata kwa watoa taarifa wakiwemo viongozi wa Serikali.
Na hivyo ujumbe uliokusudiwa kuwasilishwa kwetu wananchi unakuwa umekwamishwa na gharama za vifurushi vya data.
Wadau watoa ushauri
Wadau mbalimbali wanaishauri wizara husika, pamoja na makampuni ya simu
nchini yanayotoa huduma hiyo muhimu kwa maendeleo kuangalia upya na kwa
umakini jambo hili kwa maendeleo na tija ya nchi.
Tunafahamu kuwa Vifurushi vya Data ni Ofa za makampuni ya simu katika kufanya ushindani wa kibiashara lakini licha ya kuwa ni ofa basi tunashauri ziwe zenye kuleta unafuu kwa mwananchi kwakuwa pia kukiwa na huduma hizo nzuri, hata matumizi ya Mawasiliano kwa njia ya simu yataongezeka na kutaongeza mapato kwa Serikali kwa njia ya kodi na tozo zilizopo hivi sasa.
Imeandaliwa na baadhi ya watoa maudhui, Waandishi wa habari za mtandaoni na watumiaji wa mitandao Tanzania
Post a Comment