Uamuzi kesi ndogo ya kina Mbowe kesho




Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kesho Jumatano Oktoba 20, 2021 inatarajiwa kutoa uamuzi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.


Uamuzi huo ambao utatolewa na Jaji Mustapha Siyani (Jaji Kiongozi kwa sasa) unaweza kuwa picha ya mwelekeo wa kesi nyingine ndogo ndani ya hiyo kesi.



Kesi hiyo ndogo inahusiana na uhalali wa maelezo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adamu Hassan Kasekwa, ambayo mawakili wa utetezi waliyapinga yasipokewe kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.



Upande wa utetezi uliyapinga ukidai kuwa yametolewa nje ya muda wa kisheria na kwamba mshtakiwa huyo hakuyatoa kwa ridhaa yake bali kabla na wakati wa kuchukuliwa maelezo hayo alitishiwa na kuteswa.



Ikiwa mahakama itakubaliana na hoja za upande wa mashtaka, basi itayapokea maelezo hayo na kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.



Kupokewa kwa maelezo kutamaanisha kwamba mshtakiwa huyo amekiri makosa na hivyo mahakama itaweza kuyatumia maelezo yake hayo kumtia hatiani na kwa kuzingatia ushahidi mwingine wa upande wa mashtaka.



Lakini kama mahakama itakubaliana na hoja zote za utetezi au mojawapo kati ya hizo mbili, kuwa maelezo yalichukuliwa nje ya muda au kwamba mshtakiwa aliteswa kabla na wakati wa kutoa maelezo, basi itayatupilia mbali maelezo hayo.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post