Chibu Denis (kushoto) akiwa katika kikosi cha Taifa Stars. Kulia ni John Bocco
WAZIRI wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene, amehitimisha sakata la uraia wa Kibu Denis Prosper kwa kutangaza kumpa uraia mchezaji huyo wa Simba. Anaripoti Damas Ndembela, TUDARCo … (endelea).
Simbachawene ametumia mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 (Rejeo la 2002), kumpa uraia Kibu.
Uamuzi huo umetangazwa usiku wa Jumamosi tarehe 2 Oktoba 2021 kupitia ukurasa wa kijamii wa Twitter wa wizara hiyo uliyoweka picha ya Kibu na maneno yaliyosomeka;
“Mamlaka aliyopewa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 (Rejeo la 2002), baada ya kupokea ombi lililoletwa kwake na TFF, amempa URAIA wa Tanzania Mchezaji wa Mpira wa Miguu, Kibu Denis Prosper, Sept. 30, 2021.”
Waziri Simbachawene ametangaza uamuzi huo ikiwa imepita siku moja tangu, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kuibuka na kumtaka, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuingilia kati suala hilo akidai linatia aibu Taifa.
Mbali na Majaliwa, Zitto aliwatupia mzigo Waziri Simbachawene na Innocent Bashungwa, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo akisema, wakiamua wanaweza kuhitimisha suala hilo ndani ya siku moja.
Zitto aliibuka kuzungumzia suala hilo alipofanya mahojiano maalumu na MwanaHALISI TV na MwanaHALISI Online akishangazwa na uamuzi wa Serikali kushikilia hati ya kusafiria ya Kibu ambaye amesajiliwa Simba msimu huu akitokea Mbeya City.
Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT Wazalendo
Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) alisema, ilikuwaje Kibu akacheza Mbeya City, timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars “hakuulizwa uraia, ila amesajiliwa tu Simba anaulizwa uraia.”
Kibu anayevalia jezi namba 38 aliyopewa baada ya kusajiliwa Simba, aliicheza Taifa Stars kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi, tarehe 13 Julai 2021, uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na Stars kuibuka na ushindi wa 2-0.
George Simbachawene, Waziri wa Mambo ya Ndani
Kwenye mchezo huo, Kibu anayecheza nafasi ya ushambuliaji, alionesha kiwango kinachoridhisha na kuwezesha ushindi huo na baadaye akizungumza na waandishi wa habari alisema “nashukuru sana kwa mara ya kwanza kuichezea timu yangu ya Stars. Wazidi kunipa moyo kwani safari bado ndefu.”
Baada ya uamuzi huo wa Serikali, Zitto ameandika kwenye Instagram yake akipongeza uamuzi huo akisema “nazishukuru na kuzipongeza mamlaka za uraia.”
Post a Comment