Shahidi apiga wakili ngumi kortini kwa kumuuliza swali





AFISA wa zamani wa polisi aliyekuwa akitoa ushahidi alifungwa jela siku moja kwa kumpiga na kumuumiza wakili aliyekuwa akimuuliza maswali kortini.

Bw John Edward Njeru ambaye ni afisa mstaafu wa polisi, alisukumwa jela na hakimu mwandamizi, Bw Bernard Ochoi kwa kumtandika ngumi tumboni wakili Alex Kimani.

Bw Kimani alikuwa amesonga kwa karibu na Bw Njeru aliye na umri wa miaka 69 kumuuliza maswali katika kesi ya ulaghai inayomkabili Bw Gabriel Njoroge Mbuthia.

Bw Mbuthia ameshtakiwa kwa kughushi hatimiliki ya ardhi ya Bw Njeru iliyoko Nanyuki. Kizaazaa hicho kilisababisha mahakama kusitisha kesi.


 
Bw Kimani alisema hangeweza kuendelea na kesi kwa kuwa alikuwa anaumwa na tumbo. Bw Njeru aliyekuwa anatoa ushahidi alimtandika wakili huyo aliposongea kumuonyesha hatimiliki ya ardhi hiyo.

Shahidi huyo alipandwa na mori kwa kuulizwa maswali mfululizo na wakili huyo. Bw Kimani alikuwa amepewa idhini na hakimu aende katika kizimba cha mashahidi kumuonyesha Bw Njeru hati ya ushahidi.

Ni wakati huo ambapo shahidi huyo alikasirika na kumchapa wakili huku akimweleza kuwa alikuwa akirudia swali moja kuhusu umiliki wa ardhi hiyo.


“Kwa kuwa umevuruga utendakazi hapa kortini na kuonyesha dharau kwa kumchapa wakili akiendelea na kazi yake, nitakufunga jela siku moja,” Bw Ochoi alimweleza afisa huyo wa zamani wa polisi.

Pia hakimu huyo alilaani kitendo cha Bw Njeru cha utovu wa nidhamu na kudharau mahakama. Mawakili na kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka pia walilaani kitendo hicho cha shahidi huyo.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 15, 2021 kusubiri ripoti ikiwa Bw Njeru atafunguliwa shtaka au la.

Hakimu alimshauri wakili huyo apige ripoti katika kituo cha polisi cha Capital Hill. Bw Ochoi alimwagiza wakili huyo awasilishe ripoti ya matibabu.


 
Bw Mbuthia ameshtakiwa mnamo Julai 21, 2009 kuwa alighushi hati ya umiliki wa shamba lililoko Nanyuki.

Hati hiyo ilionyesha shamba hilo la hekta 0.0394 lilisajiliwa kwa jina la Gabriel Njoroge Mbuthia mnamo Aprili 20 2007. Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana katika kesi hiyo.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post