NI dhambi iliyoje? Mtoto mchanga wa kike mwenye umri wa miezi mitatu (Malaika wa Mungu), amenusurika kifo baada ya kuzikwa na mama yake mzazi akiwa hai (hajafa).
Mtoto huyo alikaa kwa saa 24 (siku moja) ndani ya kaburi dogo alilofukiwa na mama yake kabla ya kuokolewa na sasa yupo hai na anaendelea vizuri.
KICHANGA HAKIONEKANI
Ilikuwa wiki iliyopita ambapo katika hali ya kushtua, mama mmoja aliyedaiwa kuwa alikuwa mjamzito na kujifungua alikamatwa baada ya kuenea kwa taarifa za kutoonekana na kichanga chake ilihali watu walimuona wakati akiwa mjamzito na kusikia alijifungua.
Baada ya kuenea kwa taarifa hizo, mwanamke huyo alikamatwa na Polisi ambapo ilidaiwa kuwa alikiri kumuweka mwanawe huyo kwenye sanduku la nguo kisha kumzika kwenye kaburi dogo alilochimba nyumbani kwake huko Tsomo katika Jimbo la Eastern Cape nchini Afrika Kusini.
Mama huyo mwenye umri wa miaka 34 alikuja kutajwa jina lake la Lindiswa Ntalo baada ya kufikishwa mahakamani wiki iliyopita na kusomewa mashtaka yanayomkabili.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi katika Jimbo la Eastern Cape, Colonel Priscilla Naidu, mwanamke huyo alikamatwa baada ya kuenea kwa taarifa hizo akituhumiwa kujifungua mtoto wa kike, lakini ghafla mtoto huyo akawa haonekani.
“Alidai kumuweka mtoto wake wa kike kwenye sanduku la nguo na kumzika kwenye kaburi dogo katika makazi yake,” amesema msemaji huyo wa Polisi.
Naidu anasema kuwa, Jeshi la Polisi huko Tsomo lilipokea taarifa kutoka kwa Chifu wa Tsomo ambaye alieleza kwamba, mwanamke huyo alikuwa mjamzito na alijifungua, lakini mtoto alikuwa haonekani.
UPEKUZI/HAJAFA
Jeshi la Polisi lilikwenda kufanya upekuzi kwenye makazi ya mwanamke huyo ndipo wakaona sehemu iliyokuwa imechimbwa na walipofukua ndipo wakakuta ni kaburi dogo ambalo ndani yake kulikuwa na sanduku la nguo.
Anasema walipolifungua sanduku hilo ndipo wakamkuta mtoto huyo akiwa ameviringishiwa blanketi, lakini kubwa waliloshukuru walimkuta bado akiwa yu hai pamoja na kwamba alikuwa ameteseka mno kwa kukosa hewa.
Msemaji huyo anasema kuwa, mtoto huyo alikimbizwa hospitalini huku mama yake akitiwa mbaroni.
Baada ya mwanamke huyo kukamatwa naye alipelekwa hospitalini kwa ajili ya vipimo kisha kurejeshwa mahabusu.
Baadhi ya wanajamii wameingiwa na hofu kwamba, huwenda mwanamke huyo akakutwa na hatia ya mauaji.
ALITAKA KUTOA MIMBA
Kiongozi wa Mila, Nkosi JongisizweNgcongolo alisema; “Hii inashtua. Mama huyo alijaribu mara kadhaa kutoa mimba, lakini alijifungua na sasa amemzika akiwa hai.
“Aliwaambia ndugu zake kwamba alitaka kuitoa mimba yake. Kwa hiyo hili ni jambo alilokusudia,” alisema.
WATOTO NANE
Mama huyo, katika maelezo yake alisema kuwa, ana jumla ya watoto nane na mdogo kabisa alikuwa na umri wa miezi nane wakati anashika ujauzito huo.
“Mbali na wanangu, pia ninalea watoto wa dada yangu. Mimi peke yangu ninawalea wote hawa. Wazazi wangu wamekufa na dada yangu ameniachia watoto wake, yupo huko Gauteng (jimbo lingine),” anasema na kuongeza;
“Sina ajira, ninaishi kwa misaada ya wasamaria wema. Baba wa mtoto huyu (aliyemzika) alinikimbia na sijui alipo na alinipa mimba kwa usiku mmoja tu niliolala naye, niliwaza nimeongeza mtoto mwingine, sasa itakuwaje?”
AACHIWA KWA DHAMANA
Hata hivyo, baada ya maelezo yake hayo, mahakama imeruhusu apewe dhamana akawahudumie watoto aliowaacha uraiani wakati uchunguzi wa kesi hiyo ukiendelea.
STORI: IJUMAA WIKIENDA, DAR
Post a Comment