KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania,Taifa Stars, Kim Poulsen, amesema walikosa bahati kwenye mechi ya juzi dhidi ya Benin, hali iliyosababisha wapoteze kwa bao 1-0 kwenye mechi ya Kundi J, kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.
Stars imeondoka jana mchana kuelekea Benin na matumaini makubwa kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji wao hao.
Huku Kiungo wa Yanga, Zawadi Mauya, ameongezwa kwenye kikosi hicho akichukua nafasi ya Muzamir Yassi ambaye hatakuwepo kutokana na adhabu ya kadi mbili za njano.
Stars juzi ilipoteza kwa kukubali kichapo cha 1-0 kwa kupoteza pointi tatu muhimu, mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa Oktoba 10, 2021 nchini Benin ikiwa ni vita ya kusaka pointi tatu muhimu.
Taifa Stars iliondoka na Ndege ya Air Tanzania jana ikiwa na matumaini makubwa ya kuweza kupata ushindi licha ya kuwa mchezo huo utakuwa mgumu.
Wakati Kocha huyo akisema hayo, nahodha Mbwana Samata amewataka Watanzania kutokata tamaa kwani kuna mechi zingine tatu ambazo zinaweza kubadilisha matokeo ya msimamo wa kundi hilo.
Baada ya kumalizika mechi hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Poulsen alisema walimiliki mpira kwa kipindi kirefu na hasa kipindi cha pili, lakini kwa bahati mbaya walipoteza nafasi nyingi.
"Tumecheza vizuri, lakini hatukutumia nafasi, hasa kipindi cha kwanza, Msuva alikosa nafasi kadhaa. Kipindi cha pili tuliwashambulia sana, lakini kwa bahati mbaya tukafungwa goli lililotokana na uwezo binafsi ya mchezaji mwenye jezi namba tisa Mounie (Steve), ambaye ana uzoefu. Alifunga bao zuri na Benin walitumia nafasi hiyo tu walioipata kipindi cha pili," alisema kocha huyo.
Alisema kuwa Benin ni timu nzuri na wako namba nane kwenye viwango vya soka barani Afrika.
"Pamoja na uzuri wao kipindi cha pili tuliwashambulia sana, lakini bahati haikuwa yetu na hata wao walipopata bao, walirudi nyuma kulinda. Kuna siku unaweza kucheza na kumiliki mpira, lakini ukapoteza mechi," alisema kocha huyo raia wa Denmark.
Naye nahodha wa timu hiyo, Samatta aliwataka Watanzania kuendelea kuwaunga mkono, akisema pamoja na kupoteza, hawajakata tamaa na mapambano bado yanaendelea.
"Tukipambana, tulijitahidi, lakini hatukupata bahati ya kufunga, lakini niwasifu Benin walikuwa wazuri mno kwenye sanaa ya kuzuia, wakisaidiwa na maumbo yao makubwa na nguvu walizonazo. Lakini tumecheza mechi tatu na zimebaki tatu. Mechi zilizobaki zinaweza kubadilisha msimamo wa kundi letu, tuna mechi kwao pia," alisema Samatta.
Stars kwa sasa inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne kwenye Kundi J, Benin ikiongoza ikiwa na pointi saba, Congo DR, ikishika nafasi ya pili kwa pointi tano, Madagascar ikiwa haina pointi.
Post a Comment