Kanoute, Mkude Wapigwa Marufuku Simba SC





HUKO Simba ni mwendo wa pasi tu, hakuna kubutua kwani kocha mkuu wa kikosi hicho, Didier Gomes ameonekana akiwasisitizia viungo wake, Sadio Kanoute na Jonas Mkude kuwa watulivu wanapokuwa na mpira na kuhakikisha wanapiga pasi fupi fupi za uhakika na siyo pasi ndefu zinazopotea.

 

Hayo yote yalionekana katika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea kufanyika katika Uwanja wa Bocco Veteran, Dar, wakiwa katika maandalizi ya mchezo wa ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy utakaofanyika Oktoba 17, mwaka huu nchini Botswana.

 

Kocha Gomes katika mazoezi ya juzi Jumanne, alionekana akiwaelekeza jambo Kanoute na Mkude kuacha kupiga pasi ndefu ambazo mara kadhaa zilikuwa zikipotea na kuwasisitiza kupiga pasi fupifupi.

 

Kitendo hicho kinachukuliwa kama mbinu za kocha huyo dhidi ya wapinzani wake ambao wanasifika kwa kuwa na wachezaji bora katika eneo la kiungo jambo ambalo ni wazi anahitaji kulitawala kwa kuhakikisha wanamiliki sehemu kubwa ya mchezo.

 

Wakati huohuo, mabeki wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Israel Mwenda wameonekana kuandaliwa tayari kuwavaa Jwaneng Galaxy.

 

Juzi mabeki hao walipewa mazoezi maalumu wakiwa wamejiunga na kikosi hicho wakitokea kwenye majukumu ya timu ya taifa walipokuwa wakiitumikia Taifa Stars.

MARCO MZUMBE NA CAREEN OSCAR




0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post