Dk. Gwajima avutiwa na ‘Karibu Dodoma Festival’, atamani kuona yakiendelea ili watu watambue afya zao





WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima amesema kutokana na Karibu Dodoma Festival kuonesha mafanikio kwa watu wengi kujitokeza kupima afya zao kuna haja ya kila baada ya miezi mitatu kuwe na matamasha kama hayo kikanda lengo likiwa ni kupunguza wananchi kuchelewa kutambua magonjwa yanayowakabili.


Akizungumza jana katika uwanja wa Chinangali Park jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye maonesho ya Karibu Dodoma Festival ambayo yalikuwa ni maalum kwa ajili ya kutoa elimu juu ya kazi mbalimbali ambazo zinafanyika ndani ya Serikali, Waziri Gwajima aliwapongeza waandaaji wa tamasha hilo kwa kufanya kazi nzuri.

Amesema jambo hilo ni zuri na linafaida nyingi ambapo ametaka kila baada ya miezi mitatu kuwe na matamasha kama hayo kikanda ili kuweza kugundua matatizo ya watanzania wengi.

“Kuna faida nyingi sana naahidi huu ni mwanzo mkubwa kila baada ya miezi mitatu kanda kwa kanda, Taasisi zetu mbele, hodi waheshimiwa wakuu wa Mikoa hodi waheshimiwa wakuu wa Wilaya tushirikiane taasisi zote zinatembea zitafika huko kwa wananchi tupunguze wananchi kuchelewa kutambua magonjwa yao wakati magari yenye maabara yameishakuja.

“Mama Samia (Rais wa Tanzania) kanunu magari yanayotembea  na wataalamu wapo wengine wahawalikani twende tukawainue,”amesema.

Amesema mara baada ya kutembea mabanda amejifunza watanzania wana matatizo akitolea mfano banda la TB amekuta watu wengi wanatatizo la Kifua Kikuu.

“Mbele yetu tumejifunza matatizo yapo kwenye TB kule tumeona watu wanatembea na TB pamoja na Kisukari watu wanahitaji huduma usajili wa watoto mambo mengi kwenye bima za afya.

“Tutaratibu baada ya hapa tutampelekea Waziri Mkuu  kifanyike kikao cha tathmini tujue wapi tumefanya vizuri wapi hatukufanya vizuri lakini tuangalie tunaendelezaje hili suala liende Nchi nzima kama Wabunge ambao walikuwa ni wateja wameona.

“Tunahitaji kuwezeshwa sisi wapenda maendeleo tuanzishe kapu la pamoja ratiba itoke wasanii wapo leo mtu hapa amegunduliwa ana viashiria vya kansa ya shingo ya uzazi huyu alikuwa  hana habari alikuwa anajijua yupo salama ingemchukua muda  tayari angeaanza kwenda Ocean Road si ajabu asingefika,”amesema.

Aidha, amewashukuru watumishi wa afya kwa kufika katika tamasha hilo ambapo amedai limeonesha mafanikio makubwa na cheti alichopatiwa ni cha wote na sio cha kwake peke yake.

“Nawashukuru sana watumishi wa afya, na NGO’s zote mmefanya jambo kubwa sisi tulikuwa tunaratibu tu nawashukuru sana wasanii bila nyinyi hii Dodoma Festival isingefanikiwa.Nimepokea hichi cheti ni cha wenzangu wote katika sekta ya afya mmefanya kitu kikubwa kuziita hizi taasisi zote,nitarudisha shukrani kwa wasanii na Mkuu wa Wilaya,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri amesema walikubaliana kuwe  na sehemu moja kwa ajili ya kuwakutanisha watanzania wenye changamoto mbalimbali za kiafya ambao hawawezi kuwafikia Madaktari bingwa.

“Na kwa hiyo tuliwaomba wawakilishi wako kwenye Wizara wawe kwenye kamati na leo tunafaraja ushiriki wa Wizara ya afya una zaidi ya wawakilishi 57,”amesema Shekimweri.

Mkuu huyo wa Wilaya amemshukuru Waziri Gwajima kwa kuruhusu wataalamu wa sekta ya afya kuwepo katika tamasha hilo kwa ajili ya kuwasaidia watanzania wenye matatizo mbalimbali.

“Tunakushukuru kwa ridhaa uliyoitoa kuruhusu watu wa JK, Muhimbili kuwa hapa Benjamini Mkapa na taasisi zingine sio jambo jepesi kimaamuzi hawa ni watumishi wa umma huko walikoondoka kuna kuonana na wagonjwa tunakushukuru sana.Ninaimani tumegusa nyoyo za watu,”amesema.




0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post