NI mzaliwa kutoka mkoani Iringa, lakini baada ya muda kidogo kupita baba yake alihamishia makazi yake mkoani Morogoro kikazi. Wakati huo staa mkubwa kwa sasa kwenye gemu la Bongo Fleva, Abednego Damian almaarufu Belle 9 alikuwa bado mtoto mdogo.
Belle 9 anasema yeye ni mtoto wa pili katika familia ya watoto watatu. Ametamba na anaendelea kutamba na ngoma zake nyingi kama Masogange, Amerudi, Nilipe Nisepe, Sumu ya Penzi, Bembeleza na nyingine nyingi.
Gazeti la IJUMAA limefanikiwa kupiga naye stori mbili-tatu katika mahojiano maalum (exclusive interview) kuhusu maisha yake binafsi pamoja na kazi yake ya muziki;
IJUMAA: Mapokezi ya EP yako yakoje?
BELLE 9: Mapokezi yapo vizuri sana, namshukuru Mungu kwa hilo.
IJUMAA: EP ya Baba Boss TV ina maana gani?
BELLE 9: Mtoto wangu wa kwanza anaitwa Boss na alizaliwa Juni 9, ndiyo siku ambayo niliachia EP hiyo kama heshima kwake hivyo mimi ndiye Baba Boss mwenyewe.
IJUMAA: Umekuwa msanii ambaye unakuwa kimya kwa kipindi kirefu kisha baada ya muda unarudi, tatizo kubwa ni nini?
BELLE 9: Siyo kama huwa nakuwa kimya makusudi, hapana, kuna muda kama sina kitu muhimu cha kuposti ni bora nikae kimya au nifanye mambo mengine mpaka pale nitakapoachia kazi yangu mpya ndiyo nitaanza tena kuonekana mitandaoni.
IJUMAA: Huo utaratibu umeuanza lini?
BELLE 9: Ni utaratibu ambao nipo nao siku zote kwa wale ambao wananifuatilia, basi watakuwa wanajua nini nazungumzia.
IJUMAA: Lakini hauoni kama kwa kufanya hivyo utawapoteza mashabiki zako wengi ambao wanatamani kukuona kila wakati?
BELLE 9: Mimi naamini mashabiki zangu ni watu ambao wanapenda sana kazi zangu kuliko maisha yangu binafsi, ndiyo maana najitahidi kuwa karibu nao kila ninapoachia kazi mpya kwa sababu hata wao pia walinijua mimi kupitia kazi zangu na siyo skendo za aina yoyote ile.
IJUMAA: Kwa hiyo unawaambia nini mashabiki wako?
BELLE 9: Nawapenda sana, mimi ni msanii wao na nipo hapa kwa ajili ya kuwapa burudani nzuri hivyo wasinichoke waendelee kunisapoti.
IJUMAA: Vipi shemeji yetu mzima?
BELLE 9: Yuko poa kabisa.
IJUMAA: Umekuwa kwenye gemu kwa muda mrefu sasa na unafanya kazi nzuri sana, lakini hauonekani kimataifa zaidi kama vile kuwa ‘nominated’ kwenye tuzo mbalimbali au kuitwa kufanya shoo kubwa kama ilivyo kwa wasanii wengine; Harmonize, Diamond na wengineo, tatizo liko wapi?
BELLE 9: Ni kweli nipo kwenye gemu kwa kipindi kirefu, lakini binafsi huwa naamini katika muda, kwa sababu muda ndiyo kila kitu kwa mwanadamu mbali na hilo wakati wa Mungu ndiye wakati sahihi hivyo muda wa mimi kujulikana kimataifa zaidi ukifika, basi kila kitu kitakuwa sawa.
IJUMAA: Huoni kama ukimya wako muda mwingine labda ndiyo unafanya watu wakusahau?
BELLE 9: Hapana, haimaanishi ninavyokuwa kimya basi sionani na mashabiki wangu, siyo kweli kwa sababu kuna njia nyingi za kuwasiliana nao, naweza nikakutana nao kwenye shoo mbalimbali, mtaani na sehemu nyingine nyingi tu.
IJUMAA: Kama ulivyokiri mwenyewe kuwa umekuwa kwenye gemu kwa muda mrefu kwa nini umeamua kuachia EP na siyo albam?
BELLE 9: Albam ni kitu kizuri sana kwa sbabau ni kitu ambacho kinamtambulisha vizuri msanii, kwa upande wangu kwa sasa nimeona niachie kwanza EP kisha baadaye nitatoa albam.
IJUMAA: Kuna wasanii wengi ulianza nao, lakini kwa sasa hawasikiki tena, unadhani shida iko wapi au wanashindwa kujibrandi wao wenyewe?
BELLE 9: Siwezi nikasema kuwa wanashindwa kujibrandi kwa sababu unaweza ukafanya hivyo, lakini kama mambo yemegoma ni yamegoma tu, binafsi nimeweza kusimama mpaka sasa kwa sababu nimekomaa na kazi na kuzidi kujiimarisha zaidi.
IJUMAA: Kabla ya kuoa umeshawahi kutembea na mwanamke aliyekuzidi umri? (jimama)
BELLE 9: Sijawahi na wala sidhaani kama hicho kitu kitakuja kutokea maishani mwangu kwa sababu najiheshimu sana hivyo siwezi kutembea na mwanamke aliyenizidi umri kwa sababu siku zote nawaheshimu kama dada au mama zangu.
IJUMAA: Gemu ya muziki wa Bongo Fleva kwa sasa unaionaje?
BELLE 9: Mimi naona iko poa tu, japokuwa kuna ugumu f’lani hivi, lakini Mungu ni mwema angalau kipindi hiki kumekuwa na njia nyingi za kuuza muziki wetu tofauti na zamani.
IJUMAA: Wasanii gani ambao unawakubali na unafuatilia sana kazi zao?
BELLE 9: Wapo wengi sana, lakini kwa wachache ni Profesa Jay, Dully Sykes, Diamond na wengineo ni watu ambao tangu mwanzo walianza vizuri na bado wanafanya poa kwenye gemu.
Post a Comment