Yanga yamaliza hasira za Zanaco, yachapa mtu 3-1



BAADA ya kumaliza Tamasha la Wiki ya Wananchi na kuwatambulisha wachezaji wake wapya kwa mashabiki na kulala kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Zanaco , mchana wa leo Yanga imecheza mechi ya kirafiki dhidi ya Friends Rangers.

Katika mechi hiyo Yanga imeshida mabao 3-1. imepgwa kimya kimya katika uwanja uliopo kwenye kambi yao Avic Town Kiganboni, Yanga imechezesha mastaa wake kwa nyakati tofauti.

Kipindi cha kwanza kocha Nessredine Nabi aliwaanzisha kipa,  Eric Johora, mabeki Djuma Shaban, Shomary Kibwana, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na kijana mmoja wa U-20.

Kiungo walianza Tumombe Mukoko, na Zawadi Mauya huku mbele wakianza Yacouba Songne, Fiston Mayele, Herritier Makambo na Ditram Nchimbi.


 
yanga pic 1
Dakika 45 za kipindi cha kwanza za mchezo huo zilimalizika kwa sare ya bao 1-1, bao la Yanga likifungwa kiufundi na Mayele baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Yacouba na Friends ikasawazisha kwa mkwaju wa penalti baada ya Ninja kumchezea rafu mmoja wa washambuliaji wa Friends ndani ya boksi la 18 la Yanga.

Kipindi cha pili kilirejea kwa Yanga kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Makambo na kuingia Yusuph Athuman huku nafasi ya Yacouba ikichukuliwa na Deus Kaseke.

Yanga iliendelea kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa kuliko Friends huku muda mwingi kocha Nabi akionekana kuelekeza na dakika kama ya 55 hivi, Mauya aliumia na kuingia Adeyum Salehe aliyeenda kucheza kama beki wa kulia na Kibwana Shomari kuingia katikati.


Mabadiliko hayo yalionekana kuwa bora kwa  Yanga  na kama dakika ya 60 hivi ilipata bao la pili kupitia kwa Nchimbi aliyefunga kwa kupiga Kiki kali akimalizia pasi safi ya Kaseke.

Namna dakika zilivyozidi kwenda Friends chini ya kocha wake Herry Mzozo, ilifanya mabadiliko lakini hayakuisaidia kwani Yanga ilionekana kuwa bora zaidi kiuchezaji na kimbinu.

Zikiwa zimesalia dakika 20, mchezo huo kumalizika, Yanga ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Mayele na kuingia Jesus Moloko aliyekuwa akicheza eneo la winga zote mbili kwa kubadilishana na Nchimbi.

Na muda mchache baadae Yanga ilipata bao la tatu kupitia kwa Yusuph Athuman aliyefunga akiwa ndani ya boksi la 18 baada ya kupiga mpira wa kwanza na kupanguliwa na kipa wa Friends kisha kuuwahi na kufunga kwa shuti kali.


 
Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika saa 10:35, Yanga ilitoka uwanjani kwa kushinda bao 3-1.

Wachezaji wengine waliokuwepo kwenye benchi la Yanga ni Dickson Ambundo, Balama Mapinduzi, Paulo Godfrey, David Bryson, Farid Mussa, Yassin Mustapha, na Erick Johora.

Licha ya kwamba ni mechi ya kirafiki lakini nje ya uwanja huo kulisheheni mabosi na viongozi wa Yanga ambao walikuwa mubashara kuwashuhudia vijana wao.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mshindo Msola, Muwekezaji Gharib Said, Mhandisi Hersi Said, Haji Mfikirwa, na Mwanasheria Simon Patrick ni miongoni mwa viongozi wa timu hiyo waliokuwepo.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post