Kiongozi wa upinzani Guinea aunga mkono mapinduzi ya kijeshi
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Guinea jana ameiomba Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kutouwekea vikwazo vya kiuchumi uongozi mpya wa kijeshi nchini humo, akisema mapinduzi ya hivi karibuni yamepokelewa vyema na wananchi.
Cellou Dalein Diallo, aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba uongozi huo wa kijeshi haustahili kuwekewa vikwazo kwa sababu umekomesha hali ya kutojali sheria nchini humo.
Diallo ambaye amewania urais mara tatu dhidi ya kiongozi aliyeondolewa madarakani, Alpha Conde, bila kufanikiwa, amesema hakukuwa na njia nyengine isipokuwa mapinduzi.
Uongozi huo wa kijeshi unakabaliwa na shinikizo kali la kidiplomasia, baada ya vikosi maalumu vinavyoongozwa na Luteni Kanali Mamady Doumbouya kuchukuwa madaraka Jumapili iliyopita na kumkamata Conde.
Post a Comment