Polisi Kuchunguza Wanawake Waliodaiwa Kudhalilishwa




Wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda akisema askari wake hawahusiki kudhalilisha wanawake kwa kuwashika maungo bila ridhaa yao, Jeshi la Polisi makao makuu limesema limetuma ofisa kuchunguza malalamiko hayo na kuwataka wote wanaodai kuathiriwa kujitokeza kutoa ushahidi.
Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imesema hakuna mtu aliye juu ya sheria, na endapo ushahidi utathibitisha kwamba hayo yaliyolalamikiwa ni ya kweli, hatua stahiki zitachukuliwa.

“Kama ni Polisi taratibu ziko wazi, atashtakiwa kijeshi na kufikishwa mahakamani kulingana na sheria, kanuni na taratibu za nchi yetu.”

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana kuhusu udhalilishaji huo, Kamanda Chatanda alisema tume waliyounda imekosa uthibitisho kwamba askari hao wamehusika kwa kuwa hawakupata ushahidi.

Hivi karibuni, wananchi wakiwa katika kikao cha Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe, walidai kuwa baadhi ya askari wamekuwa na tabia ya kuwashika maungo wanawake bila ridhaa yao na kuwalazimisha kufanya mapenzi. Kutokana na madai hayo, Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) na Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo Taifa, vimetoa taarifa kuonyesha kusikitishwa na vitendo hivyo. Mjumbe wa Sekretarieti Habari na Mawasiliano Bawacha, Devotha Minja alisema wanalaani ukatili waliofanyiwa wanawake, ikiwamo kuwataka kimapenzi kwa lazima.

“Tunatarajia kuona sheria zinachukua mkondo wake mara moja,” alisema Devota kupitia taarifa hiyo.

Mkurugenzi wa Tamwa, Rose Reuben alisema wanakemea vitendo vya baadhi ya askari kutumia mabavu na kufanya ukatili wa kijinsia kwa maneno au kimwili.

Naibu Katibu, Habari na Uenezi na Mawasiliano ACT-Wazalendo Taifa, Husuna Sungura alisema mkuu wa Jeshi la Polisi anapaswa kuwawajibisha waliotajwa kwenye kura ya siri kuhusika na matendo hayo yasiyokubalika.

“Kwa mujibu wa sheria, jeshi pia linapaswa kuwa mstari wa mbele katika kukomesha matendo yote ya udhalilishaji wa kijinsia yanayofanywa dhidi yao kwa kuwachukulia hatua za kisheria wote waliobainika,” alisema.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post