Mashahidi wanne bado siri nzito kesi ya kina Mbowe




Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imetoa ulinzi kwa baadhi ya mashahidi wa washtakiwa wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ili wasitajwe hadharani kwa sasa

Amri hiyo ilitolewa jana na Jaji Mustapha Siyani anayesikiliza kesi hiyo, kufuatia maombi yaliyotolewa na kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala, wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo.

Wakili Kibatala alitoa maombi hayo baada upande wa mashtaka kutaja idadi, majina na anuani za mashahidi wake wanaotarajiwa kuitwa mahakamani hapo kutoa ushahidi.

Aliieleza mahakama kuwa upande wa utetezi unatarajiwa kuwa na mashahidi 11, wakiwamo washtakiwa wenyewe wanne, aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro.

Akitoa ombi la kutokutaja majina ya mashahidi wengine wanne ambao alidai kuwa ni muhimu, Kibatala alidai hawatatajwa kwa sasa kwa kuwa wana wasiwasi wanaweza kutishwa na taasisi za Serikali.

“Hivyo tunaomba tusiwataje kwa sasa mpaka hao washtakiwa watakapoanza kujitetea,” alisisitiza.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka sita, mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando japo hakuwa na pingamizi kuhusu ombi hilo, lakini akapendekeza suala hilo lisikilizwe chemba kabla ya kuamuriwa na mahakama.

Jaji Siyani aliahirisha kesi hiyo kwa nusu saa ili kupitia vifungu vya kisheria kabla ya kutoa uamuzi akisema suala hilo ni la kisheria, halihitaji kukurupuka kutolea uamuzi.

Akitoa uamuzi huo baada ya kukutana chemba, Jaji Siyani alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote, amekubaliana na maombi hayo.

“Mimi nimepima uzito wa hoja zilizotolewa na Wakili Kibatala, hakuna tatizo juu ya ombi hilo. Nakubaliana na hoja zake, mashahidi wanne wasitajwe majina na anuani zao kwa sasa,” alisema Jaji Siyani.

Alisema iwapo washtakiwa watakutwa na kesi ya kujibu, maombi hayo yataishia hapo kwa sababu yanahusu kutokutajwa kwa wakati huu.

Hata hivyo, alisema miongoni mwa mashahidi hao ni askari wastaafu na Serikali inaweza kuwafikia.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 16 ya mwaka 2021 ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Wanakabiliwa na jumla ya mashtaka sita, mawili ni ya kula njama ili kutenda vitendo vya kigaidi yanayowakabili washtakiwa wote wanne.

Mengine ni kufadhili vitendo vya kigaidi kwa Mbowe pekee yake, na mali za kutekelezea vitendo vya ugaidi yaani silaha (bastola) kwa Ling’wenya peke yake na sare na vifaa vingine vya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa Halfani. Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti Mosi na Agosti 5, 2020 katika Hoteli ya Aishi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro na katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha.

Vitendo hivyo vya kigaidi wanavyotuhumiwa ni kulipua vituo vya mafuta na katika maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya watu, katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza na kumdhuru aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, lengo la kupanga kutenda vitendo hivyo vinavyotishia amani na usalama wa wananchi lilikuwa kusababisha hofu kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Awali, karani wa Mahakama, Farida Suphian aliwasomea washtakiwa hao mashtaka yanayowakabili ambapo kwa mara ya kwanza waliruhusiwa kuyajibu.

Washtakiwa wote walipoulizwa na karani huyo ikiwa ni kweli walitenda makosa hayo walikana.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post