Makubwa.. Dereva Bajaji Mbaroni kwa Kubeba Wanafunzi 17 Kwa Mara Moja



Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili akiwemo mwalimu wa shule ya msingi na dereva bajaji kwa tuhuma za kuvunja sheria za usalama barabarani na kusafirisha wanafunzi 17 kwa wakati mmoja kwa kutumia bajaji.

Wanafunzi hao ni kutoka shule za awali tofauti tofauti ambao walinaswa jana Alhamisi wakiwa wamepakiwa kwenye bajaji hiyo kupelekwa shule.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei ameliambia Mwananchi leo Ijumaa Septemba 24,2021 kuwa watuhumiwa hao walikamatwa jana asubuhi katika eneo la Mabatini jijini hapa.

Amesema Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu tukio hilo na kuanza kufuatilia hadi walipowakamata watuhumiwa hao wakiwa wamewabananisha watoto hao wenye umri kati ya miaka minne hadi mitano.


"Ni kweli tumemkamata mwalimu na dereva bajaji ambao majina yao tumeyahifadhi kwa sasa, kwa tuhuma za kuwasafirisha idadi kubwa ya watoto jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa maisha yao," amesema Kamanda Matei na kuongeza:

"Tumeanza na hawa wawili na tunawafuatilia wazazi ambao wanakodi usafiri huo kuwatoa watoto shuleni na kuwarejesha majumbani ili wachukuliwe hatua."

Pia, Kamanda Matei amewaonya wazazi na walezi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kulinda usalama wa watoto kwa kuwatumia madereva bodaboda nabajaji kusafirisha watoto kwenda shuleni, kuacha kwani ni hatari kwa usalama.


Akizungumzia tukio hilo, mkazi wa Mabatini David Joseph, ameliomba Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali kwa kuwa kitendo hicho ni cha hatari na hakivumiliki.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post