Askofu Josephat Gwajima
Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima (CCM) amekwepa kujibu swali la Rais Samia Suluhu Hassan kwamba atachaja au hachanji chajo ya Corona badala yake akajielekeza kuzungumza changamoto za jimbo lake. Anaripoti Mwandishi wetu.
Hayo yameibuka leo tarehe 2 Septemba 2021, Rais Samia aliposimama katika eneo la Tegeta na kuzungumza na wananchi wakati akielekea Bagamoyo kupiga picha za kutangaza utalii.
Akiwasalimia wananchi wa Tegeta na viunga vyake, Rais Samia alimkaribisha Askofu Gwajima kisha kuhoji; “mtachaja au hamchanji! Kisha wananchi wakajibu tutachanja.
Hata hivyo, Gwajima alipokaribishwa kuzungumza na wananchi alijielekeza kuzungumzia changamoto za jimbo hilo na kukwepa kujibu swali alilouliza Rais hasa ikizingatiwa Mbunge huyo ameweka wazi msimamo wake wa kutochanja chanjo ya corona.
Akizungumza katika mkutano huo, Gwajima alimshukuru Rais Samia kwa fedha zilizoelekezwa katika jimbo hilo kutekeleza miradi mbalimbali.
Rais Samia Suluhu Hassan
Alisema wana – Kawe si kwamba wanampenda Rais Samia pekee bali wana mahaba ya dhati kwake kwa kuwa amewafanyia makubwa jimbo hilo.
“Mama Samia ni rafiki yetu, aliwahi kufungua ofisi kule Mabwepande wakati akiwa makamu wa rais, lakini alipoingia madarakani kama Rais ametupendelea wana Kawe.
“Ametupatia bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa barabara 114 kupitia Tarura, lakini kuanzia tarehe 10,15 Septemba maji kutoka Ruvu chini yataanza kusambazwa kupitia matenki yliyojengwa,” alisema.
Alisema mbali na hayo, jimbo hilo linakabiliwa na uhaba wa shule hususani katika mtaa wa Wazo.
“Kule hakuna shule kabisa kuanzia msingi na sekondari… watoto wanakwenda kusoma Kunduchi na kuhatarisha maisha yao kwani wanagongwa na magari.
“Pia kuna suala la mafuriko, ulipokuwa ukigombea mwaka jana uliahidi bilioni 5 za kumaliza tatizo la mafuriko katika eneo la Chasimba, watu wengi wamepoteza maisha katika eneo hili, hivyo tunakukumbusha mama,” amesema Gwajima.
Post a Comment