ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza, amekemea tabia ya kusifia viongozi waliopo madarakani, akishauri iwe miongoni mwa makosa ya jinai nchini, ili kupunguza watu kujipendekeza kwa lengo la kupata vyeo.
Akizungumza jana jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha mwandishi mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu, Askofu Bagonza alisema, watu wengi wanashindwa kufanya kazi walizokabidhiwa kuzifanya badala yake wanaweka nguvu kusifia viongozi.
Alisema baadhi ya viongozi wa serikali ngazi za chini wamekuwa na tabia hiyo na kumtwisha Rais mzigo ambao hastahili kutwishwa.
Askofu Bagonza alisema kielelezo kizuri ni Hayati Benjamini Mkapa aliyewahi kutamka bayana kwamba lugha nzuri ya kutumia ni kuiita serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) badala ya nadharia iliyotaka kujengwa ya Serikali ya Magufuli.
Alikumbusha kuwa Hayati Mkapa alitoa angalizo hilo mbele ya Hayati Dk. John Magufuli alipowaita na kufanya mazungumzo na viongozi wastaafu Ikulu jijini Dar es Salaam.
"Kama ni kiongozi wa chini afanye kazi yake na siyo kubakia anasifia tu Rais, yaani hata choo kikijengwa, anasema Rais ameleta hela ya kujenga choo hiki," alisema Askofu Bagonza.
Alifafanua kuwa imekuwa kawaida hata kwenye misiba mtu anasimama anasema anampongeza Rais, jambo ambalo ni baya kwa kuwa kiongozi huyo anatwishwa mizigo isiyomhusu.
Kiongozi huyo wa kiroho alifafanua kuwa ubaya wa kumsifia Rais kila mahali ni pamoja na kumfanya aone wasiomsifia katika jamii labda hawampendi, jambo ambalo siyo sahihi.
Askofu Bagonza alisema hali hiyo inawafanya viongozi wasiofanya kazi zao vizuri, waishie kumtaja na kumsifia Rais ili ionekane wamefanya kazi zao vizuri.
Pia alikemea kitendo cha viongozi kusema fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo, zimetolewa na Rais, akionya kuwa kufanya hivyo kunasababisha baadhi ya wananchi washindwe kulipa kodi za serikali wakiamini kwamba kiongozi huyo ana fedha nyingi.
Akizungumzia uchaguzi na haki za binadamu nchini, Askofu Bagonza alisema ili uwe kiongozi mzuri ni lazima jamii iliyokutuma ikuchague kwa kura zao na kwa njia halali kwa mujibu wa katiba za vyama na Katiba ya nchi.
Akizungumzia umuhimu wa kuwa na Katiba Mpya, Askofu Bagonza alisema Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema marais wazuri wanatakiwa kuongoza kwa vipindi viwili ili waondoke na uzuri wao, lakini marais wabaya wataondolewa na wananchi.
Alisema katiba nzuri ni silaha kubwa kwa wananchi kwa sababu wanaweza kuitumia kuweka madarakani viongozi wazuri na kuwaondoa katika uongozi wale wabaya muda wowote watakapotaka.
"Watanzania wanahitaji katiba yenye uwezo wa kuweka na kuwaondoa viongozi madarakani badala ilivyo kwa sasa," Askofu Bagonza alisema.
KATIBA MPYA
Katika uzinduzi wa kitabu hicho, Ulimwengu alisema amelazimika kuandika kitabu hicho ambacho kimebeba makala zake zote tangu mwaka 1996 kwa kuwa anaamini mawazo yake mpaka sasa hayajabadilika.
Alisema makala zake hata kama aliziandika zikiwa za kijiunga kwa wakati huo, lakini bado anaamini mawazo na fikra zake za wakati huo bado hazijabadilika mpaka sasa.
Kuhusu Katiba Mpya, aliwataka Watanzania kuanza kuchambua vipengele ambavyo wangependa viwamo katika Katiba Mpya hiyo ili wakipata wasaa wavijadili badala ya kusema tu wanataka Katiba Mpya kwa ujumla wake.
UBORA WA ELIMU
Akizungumzia suala la mfumo wa elimu nchini, Ulimwengu alisema bado una matatizo mengi na kwamba haumwandai mtu kutengeneza kitu cha kulisaidia taifa.
"Hakuna uwezekano wa kizazi chetu kupata maendeleo na kupiga hatua ikiwa kitaendelelea kufundishwa kwa lugha wasioijua na pia wale wanaowafundisha nao hawaijui hiyo lugha," Ulimwengu.
Katika uzinduzi huo, Ulimwengu alitia saini na kukiuza kitabu chake hicho kwa baadhi ya washiriki wakiwamo waandishi wa habari pamoja na wanaharakati kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Kitabu hicho kimepewa jina la 'Rai ya Jenerali Ulimwengu', kikiandikwa na mwandishi nguli huyo.
Post a Comment