Yanga yakamilisha usajili wa Litombo




NI rasmi sasa klabu ya Yanga imethibitisha kukamilisha usajili wa beki wa kati Yanick Bangala Litombo ambaye wataenda kumtambulisha nchini Morroco sehemu ambayo wanaenda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao.

Yanga Jumapili waliondoka nchini kwenye majira ya saa kumi jioni katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere kuelekea nchini Morroco tayari kwa kambi hiyo ya siku 10.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli alisema kuwa kikosi hiko kimeondoka kikiwa na msafara wa wachezaji 28 huku wengine wakitarajiwa kuungana nao moja kwa moja akiwemo Yacouba Songne na Kipa Diarra Djigui huku mchezaji mmoja ambaye ni Bangala Litombo wakitarajia kumtambulisha huko huko nchini Morroco.

“Kikosi kitaondoka kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya ambapo kama mnavyofahamu kuwa maandalizi hayo yatafanyika nchini Morroco, hivyo jumla ya wachezaji 28 wataondoka lakini wengine wataungana nasi hukohuko hivyo hawatakuwa katika sehemu ya msafara huo wa Yanga.

“Yacouba Songne na Kipa Diarra Djigui wao wataungana nasi huko huku pia tukitarajia kumtambulisha mchezaji wetu mpya tukiwa huko na mchezaji huyo ndiye anayetuungia usajili wetu katika dirisha hili la usajili.

“Watu wanazungumza kuhusu sisi kuongeza wachezaji wa kimataifa mara baada ya taarifa za ongezeko la wachezaji 12 wa kimataifa ila ukweli ni kwamba taarifa ilichelewa kutoka hivyo hatutaweza kuongeza mchezaji yeyote labda kupitia dirisha dogo ndio tutaweza kufanya hivyo,”alisema kiongozi huyo.

Aidha Afisa Habari huyo aliweka wazi kuwa safari ya kikosi hiko kitapitia nchini Dubai ambapo wataunganisha ndege ya kuwapeleka nchini Morroco.




0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post