Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee Profesa Abel Makubi, amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za upatikaji wa vyeti kwa kukamilisha utaratibu wa kuhama kutoka kwenye mfumo wa vyeti vya makaratasi-na kwenda mfumo wa kidijitali (Covid 19 Vaccine Electronic Certificates).
Kupitia taarifa yake aliyotoa kwa umma Agosti 8, 2021, Profesa Makubi amesema kuwa taarifa zote za usajili na vyeti kwa wale waliochanjwa zimeandikwa katika vitabu na baadae taarifa hizo zitahamishiwa katika mfumowa kielektroniki.
Prof. Makubi ameeleza kuwa Wizara ya Afya inaendelea kuratibu utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 (COVID-19) kupitia vituo vya kutolea huduma za afya vya Umma na Binafsi vilivyoidhinishwa nchini.
"Serikali inatoa tahadhari iwapo kuna watu watakao jaribu kujipatia vyeti vya chanjo kwa njia za udanganyifu, kuwa watabainiwa na mfumo na kuchukuliwa hatua za kisheria," imesema taarifa hiyo.
Ameongeza kuwa, "Ikumbukwe kuwa, wizara inafahamu mfuatano wa namba zake na zimetolewa kituo gani hivyo, ikitokea namba moja imejirudia uchunguzi utaanzia kwa watoa huduma waliotoa namba hizo na wateja wenye vyeti vya namba hizo".
Zoezi la kutoa chanjo ya UVIKO-19 lilizinduliwa Julai 28, 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambapo hadi kufikia Agosti 4, 2021 jumla ya Dozi 1,008,400 za chanjo za UVIKO-19 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa yote 26 na vituo zaidi ya 550 vya kutolea huduma za chanjo kwa Tanzania Bara.
Post a Comment