Jeshi la polisi nchini limetoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu watakaojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana kwa namna yoyote.
Julai 31 Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwataka wanachama wote ndani na nje ya Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza katika mahakama ya Kisutu siku ambayo kesi ya Mbowe itatajwa.
Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu AgostI 2,2021 Mkuu wa Jeshi la Polisi Simon Sirro amesema tuhuma dhidi ya Mbowe na wenzake ziko chini ya mamlaka ya mahakama.
“Jeshi la polisi halitegemei mtu au kikundi cha watu kwa namna yoyote kutoa shinikizo kwa mamlaka ya mahakama au kwa mtuhumiwa Freeman Mbowe aachiwe au kupewa dhamana,”amesema Sirro.
“Jeshi la polisi linatoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu kitakachojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana au namna yoyote ile kutoa shinikizo lolote,”amesema.
Ameaema jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu hao.
“Kabla ya uchaguzi nilisema kuna watu wamejipanga kulipua vituo vya mafuta na kuua viongozi wa Serikali hao wanaaopanga kuleta vurugu wajue Mbowe ni binadamu tumempeleka mahakamani tuache mahakama ifanye kazi yake.”
Sirro amewataka viongozi wa dini na taasisi nyingine ziache kusema Mbowe anaaonewa na badaala yake wasubiri mahakama iamue.
“Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza, yeye kapelekwa mahakamani tusubiri maamuzi, mikoa iliyojipanga kufanya maandamano ni kuvunja sheria.”
Post a Comment