SIMBA imeanza kwa kasi harakati zake za kusuka upya kikosi chake kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya kumalizana na nyota watatu fasta.
Simba imepania kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao baada ya kuishia hatua ya robo fainali msimu huu.
Wekundu hao wamemalizana na kipa namba moja wa Tanzania Prisons, Jeremiah Kisubi kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili kimyakimya.Prisons inayomilikiwa na Jeshi la Magereza, juzi ilimsajili kipa wa Mbeya City, Haroun Mandanda baada ya kupata taarifa za Kisubi kusaini Simba.
Simba imepanga kukifanyia maboresho machache kikosi chao katika kuhakikisha wanafanya vema katika Ligi ya Mabingwa Afrika.Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, Simba imefanikisha usajili wa kipa huyo kwa ajili ya kumpa changamoto Aishi Manula.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Simba ilifanikisha usajili wa kipa huyo haraka mara baada ya Ligi Kuu Bara kumalizika kwa kumtoa kambini saa chache huko Mbeya na kumleta jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanikisha usajili.
Alisema kuwa kipa huyo ameondolewa kambini na mabosi wa Simba kwa kumtaka azime simu yake ya mkononi kwa hofu ya kusumbuliwa na Yanga waliokuwa kwenye mipango naye.
“Prisons wametumia akili za haraka kukamilisha usajili wa kipa wa Mbeya City, Mandanda ambaye juzi walimsainisha mkataba wa miaka miwili.“
Wamechukua maamuzi hayo baada ya viongozi wa Prisons kumtafuta Kisubi kwa njia ya simu ambayo ilikuwa haipatikani, lakini kutokana na mmoja wa viongozi wa timu hiyo kupata taarifa za kuondoka kambini saa chache na kuja Dar kwa ajili ya kusaini Simba,” alisema mtoa taarifa huyo.
Simba pia imedaiwa kumsajili beki wa kulia wa KMC, Israel Mwenda, kwa mkata wa miaka mitatu.
Mwenda kwa sasa yupo nchini Sudani na kikosi cha timu ya Taifa ya U-23, ambapo Simba imemalizana naye hukohuko sambamba na straika wa Mbeya City, Kibu Daniel.
Chanzo chetu kutoka ndani ya Simba kimeliambia Championi Ijumaa kwamba, tayari uongozi wa Simba umefanikiwa kumalizana na nyota huyo, baada ya David Kameta ‘Duchu’, kutopata nafasi nyingi za kucheza mbele ya Kapombe.
“Kwa lugha nyepesi hadi sasa tayari kikosi chetu kitakuwa na mbadala sahihi wa Kapombe tofauti na mwanzo,” kilisema chanzo hicho.Pia inaelezwa kuwa tayari Simba imekamilisha usajili wa winga wa kimataifa wa Malawi, Peter Banda, ambaye anaweza kuchukua nafasi ya Luis Miquissone anayewindwa vikali na Al Ahly ya Misri.Banda, 20, kwa sasa anakipiga FC Sheriff Tiraspol inayoshiriki ligi kuu ya nchini Moldovia.
Chanzo kilisema uongozi wa Simba ulimtuma mmoja ya viongozi katika Bodi ya Wakurugenzi ambaye alikwenda kuinasa saini ya kiungo huyo
nchini Malawi.
Championi Ijumaa lilimtafuta Banda azungumzie juu ya kukamilisha usajili wake wa kujiunga na Simba ambapo alisema kuwa hawezi kusema chochote juu ya kukamilisha usajili huo ingawa aliweka wazi kuwa yupo katika mazungumzo na uongozi wa Simba.
“Ni kweli tupo katika mazungumzo na uongozi wa Simba kwa muda mrefu, kama kitatokea chochote nadhani kitafahamika huko mbeleni,” alisema winga huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alizungumzia usajili wa Simba akisema: “Tunaendelea vizuri na mipango yetu ya maboresho ya kikosi ikiwamo kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa.
“Kila kitu kinaenda vizuri, Wanasimba wanatakiwa kutulia na kusubiri waone kazi yetu inayofanywa na viongozi wao, baada ya kupokea ripoti ya kocha Gomes (Didier) na kufanyia kazi mapendekezo yake ikiwamo usajili wa wachezaji wenye kiwango kizuri na kuwa na kikosi imara.”
Post a Comment