Shahidi adai Sabaya alimnyooshea bastola mdomoni



 
Shahidi adai Sabaya alimnyooshea bastola mdomoni
SHAHIDI  wa nane katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake, Magdalena Mally au Zulfa Msangi (32), ameieleza Mahakama kuwa Sabaya alimnyooshea bastola mdomoni na kichwani na kumwambia yeye ni malaya wa kushangaza, kwani malaya huwa wanalilia fedha, lakini yeye analilia mapenzi.

Shahidi huyo alisema hayo wakati akiongozwa na Mwanasheria wa Serikali, Tumani Kweka mbele ya Hakimu Mwandamizi anayesikiliza kesi hiyo kutoka mkoani Geita, Odira Amworo katika Mahakama ya Hakimu Makazi Mkoa wa Arusha.

Alisema alionyeshwa bastola bàada ya yeye kwenda kumpigia magoti kumuomba Sabaya amsamehe na asimuue mume wake Bakari Msangi kwani yeye binafsi anaumwa na wana watoto wadogo wanaowategemea, hivyo kama amemkosea ampeleke Kituo Kikuu Cha Polisi ili aweze kushitakiwa kwa kukukosea na Mungu atambariki.

Shahidi huyo ambaye alikuwa akitoa ushahidi wake huku akilia kwa uchungu kizimbani hapo, alisema msamaha huo haukumwingia Sabaya kwani alisema kwa ukali atoke pembeni ya dirisha alikopiga makoti vinginevyo atamwaga ubongo kwa kumpiga risasi na aliogopa sana na kutetemeka na kusogea pembeni ya gari hilo la rangi nyeupe.


 
Alisema matukio yote hayo yalikuwa yakifanyika katika Lodge ya Tulia iliyopo Sakini jijini Arusha baada ya yeye kupigiwa simu na mume wake Msangi kumueleza kuwa, Sabaya amemteka na yuko hapo na kundi lake na aende mara moja na alifanya hivyo kwa msaada wa jirani yake ambaye hakumtaja jina mahakamani hapo.

Shahidi alisema alipofika Tulia Lodge majira ya saa tano usiku, alikuta makundi matatu tofauti yakiwa yamesimama na baadhi yao wakiwa na bunduki mbili, lakini muda wote simu ya mume wake Msangi ilikuwa imefungwa, hivyo iliwapa wakati mgumu hadi kufikia hatua ya kutaka kuondoka, lakini ghafla Msangi alipiga simu na kuwaeleza wasiondoke kwani yeye yuko kwenye gari nyeupe amefungwa pingu mikononi na miguuni.

Alisema wakati wote huo, Sabaya alikuwa ndani ya Lodge na hakujua yuko na akina nani baadaye alimuona Sabaya akitoka ndani huku ameshika bahasha kubwa ya khaki na akiichezea bastola yake huku akiwa na furaha.


Kwamba Sabaya alikwenda moja kwa moja katika gari yake na walinzi wake waliokuwa katika makundi wote walikimbilia magari na yeye alikimbia katika geti ili kuzuia magari na alipiga magoti na kulia kwa sauti kubwa na kumuomba Sabaya amwachie mume wake na asimuue kwani Mungu anaweza kumbariki zaidi.

Shahidi alisema ghafla waliteremka walinzi wawili katika gari nyeusi na kumburuta kwa kumshika mikono na kumuondoa na kumpeleka dirishani kwa Sabaya na aliendelea kulia huku akimuomba kutomuua mume wake kwa namna yoyote.

Alisema Sabaya aliwaruhusu walinzi wake kumshusha Msangi katika gari ili wamwongoze na kwenda kuzungumza na mke wake na walipofika katika gari, Msangi alitoa simu mbili alizoficha sehemu za siri na kumkabidhi mke wake na baadaye, walinzi walimrudisha tena kwenye gari ya Sabaya hatua ambayo mke aliendelea kulia na kuomba kwa Sabaya.

Kesi hiyo iliendelea mchana baada ya kuongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilifika hatua ya mawakili wa utetezi kumhoji shahidi katika kesi inayomkabili Sabaya na wenzake wawili Silvester Nyengu (26) na Daniel Mbura (38) katika Mahakama hiyo hiyo ya Mkoa wa Arusha.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post