Sabaya, wenzake kuanza kujitetea leo



 
Sabaya, wenzake kuanza kujitetea leo
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imesema aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake wawili wana kesi ya kujibu.

Hakimu Mwandamizi, Odira Amworo alisema jana kuwa, washitakiwa hao akiwemo Silvester Nyengu (26) na Daniel Mbura (38), wataanza kujitetea katika mashitaka ya unyang'anyi wa kutumia silaha.

Ilidaiwa mahakamani kuwa Februari 9, mwaka huu saa 11 jioni Sabaya na wenzake walivamia katika duka la Shahiid Store linalomikiwa na mfanyabiashara Mohamed Al Saad.

Mahakama ilielezwa kuwa katika uvamizi huo washitakiwa walitumia silaha wakapora mali, shilingi 3,159,000 na ili kufanikisha hilo waliwatishia kwa silaha na kuwapiga watu kwa ngumi, mateke na vibao.


 
Hakimu Amworo jana alisema alisikiliza ushahidi wa mashahidi 11 wa upande wa mashitaka na aliridhika kuwa ushahidi huo ukiwemo wa vielelezo vinane hivyo akaona kuwa washitakiwa hao wana kesi ya kujibu. 

Mashahidi upande wa mashitaka ni raia 7, polisi watatu na daktari. Shahidi wa sita katika kesi hiyo, Msangi alidai kuwa Sabaya na wenzake walivamia dukani wakiwa na bastola mbili na bunduki tano. Shahidi huyo ni Diwani wa Kata ya Sombetini jijini Arusha.

Aliwataka mawakili wa upande wa utetezi wajipange ili leo waanze kuwasilisha utetezi katika mahakama hiyo.


Mawakili Dancan Oola na Mosses Mahuna wanamtetea mshitakiwa wa kwanza, Sabaya. Mawakili Edmund Ngelema na Silvester Kahunduka wanamtetea mshitakiwa wa pili, Nyengu. Mawakili Fridolini Gwemolo na Justin Jeston wanamtetea mshitakiwa wa tatu, Mbura.

Hakimu Amworo aliwaeleza mawakili hao wawaeleze wateja wao kuwa wanaweza kujitetea wenyewe kwa kuzingatia kiapo na kuwa mashahidi.

Wakili Oola alisema Sabaya atajitetea mwenyewe na pia atakuwa na mashahidi zaidi ya wawili. Wakili Ngemela alisema Nyengu atajitetea na pia atakuwa na shahidi mmoja.

Wakili Gwemolo alisema Mbura atajitetea, atakuwa na shahidi zaidi ya mmoja na pia atakuwa na vielelezo.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post