Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ameliagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kupambana na Kukabiliana na Rushwa (Takukuru) kumkamata na kumhoji mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima ili athibitishe kauli anazozitoa dhidi ya Serikali na viongozi kuhusu chanjo ya Uviko 19.
Dk Gwajima ametoa agizo hilo leo Jumanne Agosti 17, 2021 katika Kijiji cha Kyatunge wilayani Butiama mkoani Mara, na kueleza kuwa Askofu Gwajima amekuwa akitoa taarifa za kupotosha kwa makusudi, jambo linaloivuruga wizara na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
"Gwajima ni ndugu yangu, ni shemeji yangu kabisa, lakini mimi ni waziri nimekula kiapo cha kutumikia nchi yangu sio kumtumikia shemeji yangu. Mimi ndiye msemaji wa masuala ya afya nchini, nimechoka kuvuruguwa. Naagiza akamatwe popote alipo ahojiwe juu ya haya madai yake na hatua zichukuliwe" amesema
Amesema mara kadhaa Askofu Gwajima amekuwa akitoa taarifa za kupotosha juu ya chanjo na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake, jambo ambalo limekuwa likileta mkanganyiko katika jamii.
Amesema sekta ya afya si ya kuchezewa, hivyo yeyote atakayejaribu kupotosha au kuvuruga mipango ya Serikali ni lazima achukuliwe hatua bila kujali nafasi yake au uhusiano wake na mtu yeyote.
DK Gwajima amesema Askofu Gwajima amekuwa akidai kuwa chanjo zilizoletwa nchini ni feki, hivyo ni vema aeleze chanjo feki ziko wapi.
“Nipo tayari kwenda kwa mkemia mkuu ili kupima chanjo itakayoonyeshwa na askofu huyo, ili kuthibitisha na endapo hatakuwa na imani na mkemia wa Serikali, wizara ipo radhi kwenda hata nchi jirani kwa ajili ya kupima chanjo hizo,” amesema Dk Gwajima.
Amesema mambo ya sayansi yanapingwa na sayansi, hivyo Askofu Gwajima anatakiwa kutoa uthibithisho wa kisayansi juu ya madai yake hayo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
"Watu wanasema mbona chanjo imepatikana haraka wanasahau kuwa haya mambo ni ya kisayansi, nawaomba tuukatae ugonjwa huu katika jamii kwa kukubali kuchanja, wakati wataalamu wakiendelea na tafiti kwa ajili ya chanjo ya magonjwa kama ukimwi, malaria, TB na mengine," amesema.
Post a Comment