Askofu Josephat Gwajima
RAIS wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Dk. Edward Hosea amesema Askofu Josephat Gwajima, huenda akaingia matatani, endapo kauli zake dhidi ya chanjo ya ugonjwa wa Covid -19, zitathibitika kuwa za uvunjifu wa amani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Dk. Hoseah ametoa kauli hiyo katika mahojiano na Sauti ya Amerika (VOA), alipoulizwa juu ya ufafanuzi wa kisheria dhidi ya kauli tata zilizotolewa na Askofu Gwajima wakati akipinga chanjo hiyo.
“Kawaida mtu hukatazwi kutoa mawazo yako, mtu yeyote anapaswa kutoa mawazo yake kwa jinsi anavyojiona mawazo yake yanampeleka. Isipokuwa, mawazo yake yasisabababishe uvunjifu wa amani,” amesema Dk. Hoseah.
Dk. Hoseah ameongeza “kama mimi nina haki ya kuzungumza ninachokitaka, ni sahihi katiba inanilinda lakini nisizungumze jambo likasababisha amani kuvunjika, watu wakaamua kuleta vurugu. Hivyo, ni kazi ya polisi kuhakikisha vurugu haitokei.”
Alipoulizwa kama Mbunge huyo wa Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaweza akalindwa na sheria za Bunge, iwapo atabainika kuwa na makosa, Dk. Hoseah amesema sheria haiwezi kumlinda.
Dk. Edward Hoseah, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
Rais huyo wa TLS amesema, sheria za Bunge zinaweza kumlinda endapo atatenda kosa akiwa bungeni, lakini kama atakuwa amefanya kosa nje ya mhimili huo, sheria hizo haziwezi kumlinda.
“Kulingana na sheria na kanuni za Bunge, mbunge akiwa ndani ya Bunge akifanya kazi kama mbunge analindwa na sheria na katiba, akiwa nje ya bunge akifanya kosa la jinai, sheria haiwezi kumlinda,” amesema Dk. Hoseah.
Amesema, kama Jeshi la Polisi litajiridhisha kwamba kauli za Askofu Gwajima zina viashiria vya makosa ya jina, linaweza kumchukulia hatua.
“Labda niseme kwamba, katika tasnia ya uchunguzi, sheria inafafanua mamlaka ya Polisi na namna ya kuanzisha uchunguzi, lazima ajiridhishe kwamba kinacholalamikiwa ni kosa la jinai,” amesema Dk. Hoseah na kuongeza:
“Na kama limefanyika au litafanyika, hiyo ndio test ya mamlaka ya uchunguzi katika makosa ya jinai.”
Askofu Gwajima aliingia katika mgogoro na Serikali, kufuatia hatua yake ya kupinga hadharani chanjo ya Korona, akidai kwamba hakuna utafiti uliofanyika kubaini kama ina madhara kwa binadamu au haina.
Hivi karibuni akihubiri katika Kanisa lake la Ufufuo na Uzima, lililopo Ubungo mkoani Dar es Salaam, Askofu Gwajima aliwataka wananchi wasichanjwe chanjo hiyo, kwa madai kwamba ina madhara.
Hata hivyo, Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, aliviagiza vyombo vya dola vimhoji Askofu Gwajima, ili athibitishe tuhuma zake dhidi ya chanjo hiyo.
Baada ya Dk. Gwajima kutoa agizo hilo, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema wanasubiri taarifa rasmi kwa njia ya maandishi ili watekeleze agizo hilo.
Post a Comment