Dar/ Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud amepasua jibu la uchaguzi wa marudio wa Konde na sababu zilizomfanya mgombea wa CCM kujiuzulu ubunge baada ya kutangazwa mshindi.
Uchaguzi wa Konde ulifanyika Julai 18 baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Khatib Said Haji kufariki dunia.
Uchaguzi huo ulilalamikiwa upinzani kutokana na dosari mbalimbali, mgombea wa CCM, Sheha Fakhi Mpemba alitangazwa mshindi dhidi ya Mohamed Said Issa wa ACT-Wazalendo.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza Agosti 2 aliandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo, kwa kile alichoeleza changamoto za kifamilia, jambo ambalo limepokelewa na chama chake.Jana, akiwa katika kikao cha ndani na wanachama pamoja na viongozi, Masoud alieleza namna chama hicho kilivyoshughulikia sintofahamu ya uchaguzi wa Konde.
“Nilimuandikia kwa maandishi Rais wa Zanzibar (Dk Hussein Mwinyi), kuwa Pandani lilitokea hivi, Konde likitokea kama hili, tutakuwa tumeharibu na hatutakubali kuharibu. Siku nne kabla ya uchaguzi nilifunga safari ya kumfuata Rais Samia Suluhu Hassan, nikamwambia Konde kuna taarifa za uhakika kuwa kutaharibika.
“Nikamwambia kwenye hili, tutakuwa tumechafuka, akanielewa na namshukuru kwa uungwana wake, akaniahidi kuchukua hatua kuzuia yasitokee,” alisema Masoud ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo.
Alisema siku ya uchaguzi, waliwakumbusha pia viongozi wakuu kuhusu yanayojiri Konde, huku akidai wakati mwingine taarifa za kinachotaka kufanyika dhidi ya ACT-Wazalendo, wanazipata kutoka kwa watu wema wa ndani ya CCM. Othman alisema siku zilizofuata baada ya kukamilika kwa uchaguzi, alionana na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa Serikali na CCM Pemba. Katika kikao hicho ACT-Wazalendo walieleza mapendekezo yao na CCM walitoa ya kwao kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Konde. “Walieleza namna ya kutoka katika suala hili, na sisi tukaeleza njia mwafaka ya kutoka bila shida.
Tukawaambia hii mimba imetunga nje ya mfuko, hakuna namna inabidi ifanyiwe operesheni, itolewe na itungwe nyingine.
“Nikisema hivi nadhani mnanifahamu, haina haja ya kuzunguka, hii inajulikana kama imetunga nje ya mfuko wa uzazi dawa yake itolewe. Wakaomba muda wa kuzungumza na viongozi wenzao,” alisema Othman.
Alisema walipata wito wa Rais Samia wa kuonana naye Unguja na alikwenda yeye, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Zanzibar Juma Duni Haji na Naibu Katibu (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui.
Wengine ni Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Salim Biman na mwanasheria wa ACT-Wazalendo Omar Said Shaaban.
“Tukamueleza kuwa hatukukwama labda hatukueleweka. Tukamwambia njia na hoja zetu ni hizi kama tulivyoeleza Pemba hatuna cha kubadilisha.
“Tulifikia mwafaka kuwa watakwenda kukaa na kuchukua hatua, hatua ndiyo hii mliyoiona, operesheni imefanywa tumesema tulieleze hili pengine hakukuwa na haja ya kulizungumza. Lakini tunasema ili dunia itusikie,kama ni changamoto za kifamilia sawa,” alisema Othman.
Akizungumzia suala hilo, Faki alisema hayo ni maoni yao na kuhoji iwapo chama kingehusika katika kujiuzulu kwake kwa nini alikiandika barua ya kujiuzulu.
Alipotafutwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Catherine Nao alisema, “mimi hata sifahamu kwa kweli” alijibu kwa kifupi Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdulla Juma Mabodi alisema, “... suala la kujiuzulu ni kama mlivyoona barua kwamba amejiuzulu kutokana na sababu za kifamilia na msemaji wetu mkuu wa chama (Shaka Hamdu Shaka) alishasema.”
Post a Comment